• HABARI MPYA

  Tuesday, February 13, 2018

  RAIS MAGUFULI KUKUTANA NA INFANTINO, SERIKALI NA TFF ZAJIPANGA KUUPA MAPOKEZI MAZURI MSAFARA WA FIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli atakutana na Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Giovanni Vincenzo ‘Gianni’ Infantino atakayewasili nchini wiki ijayo.
  Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrisons George Mwakyembe katika Mkutano na Wahariri wa vyombo vya Habari Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam leo mchana.
  Waziri Mwakyembe amesema, hata ikitokea dharula ya kumkosesha nafasi Mheshimiwa Rais Magufuli kukutana na msafara wa Infantino, atawakilishwa na ama Makamu wake Rais, Mama Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu, Dk. Kassim Majaliwa.
  Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrisons Mwakyembe (kushoto) akizungumza na Wahariri wa vyombo vya Habari Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam leo mchana. Kulia ni Mkurugenzi wa Wizara, Yussuph Singo na katikati na Rais wa TFF, Wallace Karia
  Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga (katikati) akizungumza kuhusu ziara ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino

  Mwakyembe amesema Serikali imejipanga kuupa mapokezi mazuri msafara wa Infantino ambaye ataongozana na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad.
  Waziri Mwakyembe amesema kwamba Serikali imeona ugeni huo ni mzito na haiwezi kuliachia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) peke yake kuratibu ziara hiyo. 
  “Kwa sababu hiyo tumeona tufanye kazi bega kwa bega na TFF ili kuhakikisha Infantino na msafara wake wanafurahi ziara hiyo,”amesema Mwakyembe, ambaye ni Mbunge wa jimbo la Kyela kwa tiketi ya chama tawala, CCM.
  Aidha, Waziri Mwakyembe amesema kwamba atahakikisha msafara huo ukiwa nchini pamoja na ratiba zake, lakini unapata fursa ya kukutana na Waandishi wa Habari.
  Infantino anatarajiwa kuwasili nchini Februari 20 pamoja na makamu wake Mkuu, David Chung na viongozi wengine wakiwemo wa mabara, Salman Bin Ibrahim Al-Khalifa, Aleksander Ceferin, David Gill, Alejandro Dominguez, Victor Montagliani na Katibu Mkuu, Fatma Samoura.
  Kwa mujibu wa Rais wa TFF, Wallace Karia, ujumbe huo unakuja kwa ajili ya Semina maalum ya FIFA itakayohusisha nchi 21, wakiwemo wenyeji, Tanzania, ambayo itadumu hadi Februari 23.
  Mapema Rais wa TFF, Karia alizungumzia namna walivyojipanga vizuri kwa ziara hiyo na akasema hayo ni matunda ya uongozi wake mzuri ulioivutia FIFA hadi kuja kuuleta mkutano huo Tanzania.
  Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Chilla Tenga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati mbalimbali za CAF amesema kwamba ugeni unaokuja nchini ni wa wasimamizi wakuu wa mchezo wa mpira wa miguu. 
  “Tuwaonyeshe tumefurahia ujio wao, wamekuja kwetu kwa sababu ya imani, wameona Watanzania wanapenda mpira wanathamini mchango wa FIFA na CAF na wanakwenda sawa na imani yao,”. “Wangependa kuona soka ya vijana na kinamama zinaendelea, wangependa kuona kuna nidhamu katika uongozi, haswa nidhamu ya matumizi ya fedha. Hayo yanafanana na sera za nchi yetu kwa sasa,”amesema Tenga, sentahafu na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kusistiza Infantino apatiwe mapokezi yanayostahili na ya heshima.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS MAGUFULI KUKUTANA NA INFANTINO, SERIKALI NA TFF ZAJIPANGA KUUPA MAPOKEZI MAZURI MSAFARA WA FIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top