• HABARI MPYA

    Saturday, February 24, 2018

    BEKI MZIMBABWE WA AZAM FC BRUCE KANGWA ASEMA LEO LAZIMA WAIFUNGE KMC CHAMAZI ASFC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BAADA ya Azam FC, kushindwa kupata ushindi kwenye mechi tatu zilizopita, beki kisiki wa kushoto wa timu hiyo, Bruce Kangwa, amewahakikishia mashabiki kuwa wataanza na matokeo ya ushindi kuanzia leo  dhidi ya KMC katika mechi ya Hatua ya 16 Bora michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) Uwanja wa Azam Complex kuanzia Saa 1.00 usiku.
    Azam FC haijashinda mechi hata moja kati ya tatu zilizopita ambazo zote zilikuwa za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikitoka sare mbili dhidi ya Kagera Sugar 1-1 na Lipuli 0-0, baada ya kufungwa 1-0 na Simba SC.
    Lakini timu hiyo bado ipo katika vita ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo ikiwa na pointi 35 kwenye msimamo, ikizidiwa pointi mbili na Yanga iliyo nafasi ya pili na Simba ipo kileleni ikiwa nazo 42, huku timu hizo mbili za juu kila mmoja akiwa na mchezo mmoja mkononi.

    Bruce Kangwa (kulia) amewahakikishia mashabiki wa Azam FC ushindi ushindi dhidi ya KMC leo  

    Beki huyo Mzimbabwe anayeweza kucheza kama kiungo pia, Kangwa amewaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi huku akiahidi kwa niaba ya wachezaji wenzake kuwa wamewaandalia mambo mazuri ikiwemo kuibuka na ushindi katika mchezo huo.
    “Ninachoweza kusema nashukuru sana kwa sapoti yenu na asante kwa kila kitu tunathamini sana kila kitu mnachofanya kwa ajili yetu. Tunafanya kazi kwa bidii kwa ajili ya mechi ya Jumamosi (kesho) kila mtu anaangalia mbele na kupambana kushinda mechi hiyo ya Jumamosi,” alisema.
    Hii itakuwa mara ya pili timu hizo kukutana, baada ya awali Azam FC kushinda 1-0, bao pekee la beki na Nahodha Msaidizi, Aggrey Morris kwa penalti katika mechi ya kujiandaa na msimu huu.
    Mabingwa hao mara nne wa Kombe la Mapinduzi, wamefika hatua hiyo baada ya kuichapa Shupavu ya Morogoro mabao 5-0, yaliyofungwa na mshambuliaji Paul Peter aliyepiga ‘hat-trick’ huku Idd Kipagwile na Yahya Zayd, nao wakitupia, KMC yenyewe iliichapa Toto Africans 7-0.
    Azam FC kihistoria hadi sasa imeshacheza mara mbili michauno hiyo tokea irudishwe tena mwaka 2015, na mara zote kikifika hatua za mbali, msimu wa 2015/2016 kikifika fainali na kupoteza kwa kufungwa ya Yanga mabao 3-1 huku msimu uliopita kikiishia nusu fainali baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba.
    Msimu wa 2015/2016 wakati kikifika fainali na kufungwa na Yanga, Azam FC ilikutana na Panone ya mjini Moshi kwenye hatua ya 16 bora katika mechi ngumu iliyofanyika Uwanja wa Ushirika, ambapo matajiri hao walitoka nyuma na kushinda mabao 2-1, yaliyofungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, beki Pascal Wawa na mshambuliaji Allan Wanga.
    Aidha msimu uliopita kwenye hatua ya 16 bora iliitoa Mtibwa Sugar kwa kuipa kipigo cha 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, bao likifungwa na winga Ramadhan Singano 'Messi' aliyepokea pande safi kutoka kwa kiungo machachari Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
    Safari hii msimu huu, mabingwa hao wa Ligi Kuu msimu 2013/2014 wanaodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji Safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, wamefika tena hatua hiyo ya 16 bora na watacheza dhidi ya KMC iliyopanda daraja, Azam FC ikiwa na kila sababu ya kusonga mbele kutimiza lengo la kutwaa taji hilo na kurejea kwenye michuano ya Afrika.
    Mbali na bingwa wa michuano hiyo kutwaa Kombe, medali na pesa taslimu Sh. Milioni 50, pia atakata tiketi ya moja kwa moja kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2019.
    Mechi nyingine ya ASFC leo; Singida United wanawakaribisha Polisi Tanzania Uwanja wa Namfua mjini Singida na kesho; Maji Maji wataikaribisha Yanga Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Buseresere FC watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza na JKT Tanzania watamenyana na Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
    Mechi za 16 Bora ya ASFC zitakamilishwa Jumatatu ya Februari 26, Kiluvya United wakiwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani na Stand United watakuwa wenyeji wa Dodoma FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BEKI MZIMBABWE WA AZAM FC BRUCE KANGWA ASEMA LEO LAZIMA WAIFUNGE KMC CHAMAZI ASFC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top