• HABARI MPYA

    Sunday, February 25, 2018

    REKODI NZURI YA SIMBA SC MICHUANO YA KIMATAIFA HAIKULETWA NA MIUJIZA

    YAPO mambo ya kubishania, lakini si uzuri wa rekodi ya klabu ya Simba kwenye michuano ya Afrika, wengi wamezoea kusema michuano ya kimataifa.
    Unapowadia mjadala wa klabu yenye rekodi nzuri nchini kwenye michuano ya Afrika, jina la Simba litachukua nafasi kubwa pasi na shaka.
    Simba ndiyo klabu pekee Tanzania iliyofika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika, mwaka 1974 ikiitoa timu ngumu ya Ghana katika Robo Fainali, Hearts Of Oak kwa jumla ya mabao 2-0.
    Yalikuwa ni mabao ya Adam Sabu (sasa marehemu) na Abdallah 'King' Kibadeni, mjini Accra, yaliyoipa timu hiyo ushindi wa 2-0, kabla ya kuja kumalizia kwa sare ya bila kufungana nyumbani mjini Dar es Salaam.
    Katika Nusu Fainali, Simba SC ilianza na ushindi wa 1-0 mjini Dar es Salaam dhidi ya Mehala El Kubra, kabla ya kwenda kufungwa 1-0 pia na Waarabu hao mjini Cairo, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako Wekundu wa Msimbazi waling'olewa.
    Baadhi ya nyota wengine wa Simba wakati huo walikuwa ni kipa Athumani Mambosasa, mabeki Shaaban Baraza, Mohamed Kajole, Athur Mwambeta, Omari Chogo, viungo Khalid Abeid, Willy Mwaijibe, Haidari Abeid, Abbas Dilunga na washambuliaji Adam Sabu na Abdallah Kibadeni.
    Simba pia ni klabu pekee ya Tanzania, iliyocheza fainali ya michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Hiyo ilikuwa ni mwaka 1993, ilipofanikiwa kutinga fainali ya Kombe la CAF, (sasa limeunganishwa na Kombe la Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho) na kufungwa na Stella ya mjini Abidjan, Ivory Coast.
    Bahati haikuwa yao Wekundu wa Msimbazi, kwani baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana ugenini, wengi waliamini kwenye mechi ya marudiano, Stella hawatapona Dar es Salaam, lakini matokeo yake, wenyeji walilala 2-0 kwa mabao ya Boli Zozo.
    Klabu hiyo pia ilifanikiwa kuwa ya pili Tanzania kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, baada ya Yanga kuwa ya kwanza mwaka 1998. Lakini Simba ilitinga hatua hiyo kiume zaidi, ikiwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek ya Misri, kwa mikwaju ya penalti.
    Hiyo ilifuatia ushindi wa 1-0 mjini Dar es Salaam, kabla ya kwenda kufungwa 1-0 na yenyewe pia Cairo, lakini mchezo ulipohamia kwenye mikwaju ya penalti, Juma Kaseja, mtaalamu wa kuokoa michomo hiyo, aliibeba Simba baada ya kucheza penalti mbili.
    Nyota waliokuwa wakiunda kikosi cha Simba mwaka 2003 ni Juma Kaseja, Amri Said, Said Sued, Boniface Pawasa, Ramadhan Wasso, Victor Costa, Yusuf Macho, Athumani Machuppa, Jumanne 'Shengo' Tondola, Emmanuel Gabriel, Steven Mapunda, Madaraka Selemani, Ulimboka Mwakingwe, Patrick Betwel, Selemani Matola, Amani Mbarouk, Farouk Ramadhan, Yahaya Akilimali, Primus Kasongo, Abu Amrani, Kevin Mhagama, Majuto Komu, Lubigisa Edward Lubigisa, Christopher Alex, William John, Emmanuel Kingu, Edibilly Lunyamila na Clement Kahabuka.
    Baada ya kukosekana kwa miaka minne kwenye michuano ya Afrika, hatimaye timu yenye rekodi nzuri zaidi nchini kwenye michuano hiyo, Simba SC imerejea mwaka huu ikishiriki Kombe la Shirikisho, ambalo mwaka 1993 walifika fainali enzi hizo ikijulikana kama Kombe la CAF kabla ya kuunganishwa na Kombe la Washindi kuwa Shirikisho.
    Mara ya mwisho Simba SC kushiriki michuano ya Afrika ilikuwa mwaka 2012 na ikatolewa Raundi ya Kwanza tu na Recreativo do Libolo ya Angola kwa jumla ya mabao Simba 5-0, ikifungwa 1-0 Februari 17 Dar es Salaam na 4-0 ugenini Machi 3.
    Simba SC iliyo chini ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mrundi, Masoud Juma, Mtunisia, Mohammed Aymen Hbibi kocha wa mazoezi ya viungo na Muharami Mohamed ‘Shilton’, kocha wa makipa, imeanza vyema kwa kuitoa Gendarmerie Tnale ya Djibouti kwa jumla ya mabao 5-0, ikishinda 4-0 Dar es Salaam na kwenda kushinda 1-0 Djibouti City.
    Simba SC sasa watamenyana na El Masry ya Misri katika Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho, mechi ya kwanza ikichezwa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Machi 7, kabla ya timu hizo kurudiana Machi 16 Uwanja wa Port Said mjini Cairo.
    El Masry inayofundishwa na gwiji wa soka wa Misri, Hossam Hassam iliitoa Green Bufalloes ya Zambia kwa jumla ya mabao 5-2, ikishinda 4-0 Cairo na kufungwa 2-1 Lusaka.
    Rekodi nzuri ya Simba pekee kwenye michuano hii inafaa kutangulizwa kama silaha kuelekea kwenye mechi na El Masry, kwa sababu moja kubwa; itawajengea wachezaji hali ya kujiamini.
    Lakini pamoja na hayo, silaha nzuri na kubwa zaidi ni maandalizi ya kisayansi ya ndani na nje ya Uwanja ukiachilia mbali hilo la kujivunia rekodi.
    Simba wanapaswa kurejea mafanikio yao ya wakati wote walipotamba kwenye michuano ya Afrika, ikiwemo mwaka 1974, 1993 na 2003 utaona walitoka kwenye maandalizi mazuri, kwa kuanzia kuunda vikosi vizuri na baadaye kufanya maandalizi mazuri ya kisayansi.
    Mwaka 1993 timu ilikwenda kuweka kambi nchini Ufaransa kabla ya mchezo wa marudiano wa Robo Fainali na USM El Harrach nchini Algeria na matunda ya ziara hiyo ni pamoja na kumalizia vizuri mchezo wa marudiano wakifuzu kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya kufungwa 2-0 wakitoka kushinda 3-0 Dar es Salaam yalikuwa pia ni kuitoa na timu ngumu Atletico Sports Aviacao ya Angola katika Nusu Fainali, wakishinda 3-1 na sare ya 0-0 ugenini.
    Mwaka 2003 kabla ya kwenda kwenye mchezo wa marudiano na Zamalek walikwenda kuweka kambi nchini Oman kwa wiki moja, baada ya maandalizi mazuri kwenye mchezo wa kwanza pia Dar es Salaam. 
    Kwa sababu hiyo, wakati Simba wanapojivunia rekodi yao nzuri kwenye michuano ya kimataifa, wakumbuke ilitokana na maandalizi mazuri pia. Ni hayo tu. Naitwa Mahmoud Zubeiry. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: REKODI NZURI YA SIMBA SC MICHUANO YA KIMATAIFA HAIKULETWA NA MIUJIZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top