• HABARI MPYA

    Saturday, February 24, 2018

    AZAM FC NAYO YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA TFF IKIIFUMUA 3-1 TIMU MPYA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Azam FC imetinga Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuichapa KMC mabao 3-1 usiku huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Iliwachukua dakika 26 tu Azam FC kuweza kupata mabao yote matatu yaliyoipa ushindi, alianza kiungo Frank Domayo dakika ya kwanza akifunga bao la uongozi kwa shuti zuri akimalizia pasi Joseph Mahundi aliyepenyezewa mpira na Yahya Zayed,
    Dakika tano baadaye mshambuliaji Mbaraka Yusuph, aliyekuwa kwenye kiwango kizuri aliipatia Azam FC bao la pili kwa shuti la ufundi akitumia vema pasi ya Zayed.
    Zayed ambaye alipika bao la pili, aliweza kuhitimisha ushindi huo baada ya kuipatia bao la tatu Azam FC akimalizia pasi safi ya kiungo Domayo.
    KMC itakayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao, ilijitutumua na kujipatia bao la kufutia machozi kupitia kwa Mohamed Hassan, aliyepiga kichwa na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko kwa Azam FC kuongoza kwa mabao 3-1.
    Kipindi cha pili Azam FC ilijitahidi kulinda ushindi ilioupata kipindi cha kwanza, ambapo KMC ilionekana kutawala mchezo lakini ilishindwa kufurukuta mbele ya safu ya ulinzi ya matajiri hao chini ya Nahodha Msaidizi, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, David Mwantika na Bruce Kangwa.
    Kwa matokeo hayo, Azam FC hivi sasa inasubiria kupangiwa mpinzani wake kwenye hatua ya robo fainali na waandaji wa michuano hiyo, itakayofanyika wiki ijayo mara baada ya mechi zote za hatua ya 16 bora kukamilika.
    Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Jumapili kabla ya kuanza maandalizi ya kuikabili Singida United katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi ijayo saa 1.00 usiku.
    Kwa ushindi huo, Azam FC inakuwa timu ya tatu kwend Nane Bora baada ya Singida United iliyoitoa Polisi Tanzania jioni ya leo kwa kuifunga mabao 2-0 Uwanja wa Namfua, Singida na Njombe Mji FC iliyowatoa Mbao FC Jumatano kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1.
    Hatua ya 16 Bora ya ASFC itaendelea kesho Maji Maji wakuikaribisha Yanga Uwanja wa Maji Maji mjini Songea kuanzia Saa 10:00 jioni, baada ya Buseresere FC kumenyana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza kuanzia Saa 8:00 mchana na Saa 1:00 usiku, JKT Tanzania watamenyana na Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
    Mechi za 16 Bora ya ASFC zitakamilishwa Jumatatu ya Februari 26, Kiluvya United wakiwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani Saa 8:00 mchana na Stand United watakuwa wenyeji wa Dodoma FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga Saa 10:00 jioni.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razak Abalora, David Mwantika, Bruce Kangwa, Yakbu Mohammed, Aggrey Morris, Stephane Kingue/Salmin Hoza dk72, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo, Yahya Zayed, Mbaraka Yusuph/Shaaban Idd dk79 na Joseph Mahundi.
    KMC; Abdul Juma, Godfrey Sabas, Juma Jabu, Rashid Mangula, Agustino Samson, Reymond Mgungila, Emanuel Memba, Abdulhalim Humud, Michael Chinedu, Adam Kingwande na Cliff Anthony.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC NAYO YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA TFF IKIIFUMUA 3-1 TIMU MPYA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top