• HABARI MPYA

    Thursday, February 22, 2018

    INFANTINO AMUAHIDI WAZIRI MKUU MAJALIWA FIFA ITALETA UWEKEZAJI MKUBWA TANZANIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Giovanni Vincenzo ‘Gianni’ Infantino ameahidi kuwekeza katika miradi ya maendeleo ya mchezo huo nchini Tanzania.
    Mtaliano huyo ametoa ahadi hiyo leo katika mkutano wake maalum na Waziri Mkuu, Dk. Kassim Majaliwa ofisini kwa waziri huyo, Magogoni mjini Dar es Salaam.
    Infantino amesema kwamba FIFA italeta uwekezaji mkubwa nchini Tanzania hususan katika miundombinu na programu nyingine za maendeleo zitakazoinufaisha Dar es Salaam na mikoa mingine tisa.
    Pamoja na hayo, infantino ameishukuru Serikali kwa ukarimu wake na kumuomba Waziri Mkuu Majaaliwa kufikisha salamu za shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa mapokezi mazuri.
    Rais wa FIFA, Gianni Infantino (kushoto) akimkabidhi Waziri Mkuu, Dk. Kassim Majaliwa (kulia) jezi maalum leo mjini Dar es Salaam 
    Waziri Mkuu, Dk. Kassim Majaliwa (kulia) akimkabidhi Rais wa FIFA, Gianni Infantino (kushoto) zawadi ya kinyago
    Waziri Mkuu, Dk. Kassim Majaliwa (kulia) akimsikiliza Rais wa CAF, Ahmad

    Infantino mwenye umri wa miaka 47, aliye katika mwaka wake wa pili tangu achukue nafasi ya Mswisi Joseph ‘Sepp’ Blatter Februari 26 mwaka 2016 ameunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kupambana na rushwa katika sekta ya michezo.  
    “Shirikisho la sola la Kimataifa linapigana pia vita dhidi ya rushwa, ni kwa sababu mapambano haya ni muhimu kwa maendeleo ya mchezo,”amesema Infantino, Katibu wa UEFA tangu mwaka 2009 na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Marekebisho ya FIFA baada ya kung’olewa kwa Blatter kwa tuhuma za ufisadi. 
    Awali ya hapo, Waziri Mkuu Dk. Majaliwa alisema Serikali inaunga mkono juhudi za FIFA katika kuleta meandeleo kwenye mchezo wa soka duniani.   
    “Serikali yetu inaunga mkono juhudi za FIFA katika kupambana na rushwa kwenye soka pamoja na matumizi mabaya ya fedha na madaraka,”amesema.
    Waziri Mkuu Majaliwa pia amelishukuru Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kuipa Tanzania uenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 na kuahidi kwamba Serikali itahakisha michuano hiyo inakuwa ya mafanikio.
    Infantino aliwasili nchini jana na viongozi wengine akiwemo Ahmad, kwa ajili ya Semina maalum ya FIFA iliyofanyika leo ikishirikisha nchi 21, wakiwemo wenyeji, Tanzania na anatarajiwa kuondoka baadey usiku wa leo kwa ndege yake maalum.
    Naye Rais wa CAF, Ahmad aliyeambatana na Infantino katika ziara hiyo ya ofisini kwa Waziri Mkuu, aliishukuru FIFA  kwa kuipa Tanzania nafasi ya kuwa mwenyeji wa semina hiyo kubwa ambayo imeisogeza Tanzania katika ramani ya soka ya dunia.
    Ahmad pia amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa ukarimu wake mkubwa kwa msafara wa FIFA tangu uwasili nchini.  
    Waziri Majaliwa alimaliza kwa kuwakabidhi zawadi za vinyago wote, Infantino na Ahmad, ambao nao walimkabidhi zawadi pia. Infantino alimkabidhi Majaliwa jezi namba tisa ya kikosi maalum cha timu ya FIFA na akampa jezi nyingine kwa ajili ya Rais Magufuli. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: INFANTINO AMUAHIDI WAZIRI MKUU MAJALIWA FIFA ITALETA UWEKEZAJI MKUBWA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top