• HABARI MPYA

  Friday, February 16, 2018

  BOCCO ANAENDELEA VIZURI BAADA YA KUUMIA JANA SIMBA IKIBANWA SHINYANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Simba SC, John Raphael Bocco anaendelea vizuri baada ya kuumia jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.
  Bocco aliifungia Simba bao la kuongoza dakika ya tisa kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Shiza Kichuya baada ya yeye mwenyewe kuchezewa rafu na Iddy Mobby nje kidogo ya boksi.
  Lakini dakika ya 29 Bocco akatolewa nje baada ya kumia na mwishoni mwa mchezo timu hizo zikamaliza kwa kufungana mabao 2-2, bao la pili la Simba likifungwa na Mganda, Emmanuel Okwi wakati mabao ya Mwadui FC yalifungwa na beki David Luhende na mshambuliaji, Paul Nonga.
  John Bocco anaendelea vizuri baada ya kuumia jana dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga

  Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe amesema leo kwamba Bocco na akifika Dar es Salaam atafanyiwa vipimo vingine ili kujua atakuwa nje kwa muda gani.
  Gembe amesema kwamba hawatarajii kumkosa Bocco kwa muda mrefu, kwa sababu anaonekana yuko vizuri kwa sasa. Amesema majeruhi wa muda mrefu katika timu ni mmoja tu, Haruna Niyonzima pekee.

  Kikosi cha Simba kinarejea leo Dar es Salaam kwa ndege baada ya sare ya jana Shinyanga na kujiandaa kwa safari ya Djibouti Jumapili kwa ajili ya mchezo wa marudiano hatua ya awali Kombe la Shirikisho Afrika Jumanne.
  Timu ya kocha Mfaransa Pierre Lechantre itakuwa na kazi nyepesi katika mchezo wa marudiano Djibouti City Jumanne baada ya ushindi mnono wa mabao 4-0 kwenye mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam Jumapili iliyopita.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BOCCO ANAENDELEA VIZURI BAADA YA KUUMIA JANA SIMBA IKIBANWA SHINYANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top