• HABARI MPYA

    Wednesday, May 10, 2017

    KWA NINI MAKOCHA WAKUU WANAKWEPA MIKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    “Nimesikitishwa na matokeo, si uchezaji. Nimependa uchezaji binafsi na pia uchezaji wa pamoja. Tumefungwa kwa sababu hatukufunga bao na tulipata nafasi nzuri za kufunga kabla ya wao. Walikuwa wana bahati na lile goli,”
    “Siwezi tena kuwauliza wachezaji wangu, nani hajacheza hata dakika kwa wiki kadhaa - Phil Jones, Chris Smalling na Juan Mata wote walikuwa vizuri. Timu ilikuwa vizuri, iliyojipanga, tulijaribu kushinda, tulicheza kushinda, tulijilinda vizuri na Arsenal hawakuwa wazuri kuliko sisi kwa maoni yangu,”.
    Hayo ni maneno yake kocha Mreno wa Manchester United baada ya kipigo cha mabao 2-0 wiki iliyopita kutoka kwa wenyeji, Arsenal kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England.  

    Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina hatokei kwenye mikutano na Waandishi wa Habari

    Ni utaratibu wa kawaida kila baada ya mchezo katika Ligi kubwa na mashindano mbalimbali, makocha wakuu huelekea kwenye chumba cha mikutano na Waandishi wa Habari kuzungumza.
    Kwa Watanzania wanaofuatilia Ligi mbalimbali za Ulaya, hususan ya England na Hispania, La Liga zinazoonyeshwa moja kwa moja nchini wamekuwa wakijionea makocha na Manahodha wao wakizungumza kila baada ya mechi.
    Waandishi wa Habari wanajitokeza kwenye chumba cha mikutano kuwasikiliza makocha wanazungumzia mechi kwa matokeo mabaya au mazuri kwa timu zao.
    Mashabiki walioshuhudia mchezo kwa matokeo mabaya, au mazuri wanapata nafasi ya kutuliza vichwa kwa majibu ya kitaalamu ya makocha wao kuhusu mchezo watakayoyasikia kupitia vyombo vya Habari.  
    Lakini mambo ni tofauti kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambako wakati bado tunavumilia kero ya makocha kuvaa ovyo linajitokeza pia la kukiukwa au kupuuzwa kwa taratibu muhimu.
    Moja ya taratibu ambazo zinakiukwa na kupuuzwa ni Makocha Wakuu kuzungumza kila baada ya mechi.
    Kwa mujibu wa utaratibu, makocha wakuu wanapaswa kuzungumza kila baada ya mechi, lakini sasa ni makocha wasaidizi ndiyo wanaozungumza baada ya mechi.
    Ilianza taratibu, makocha wa klabu kubwa, Simba na Yanga ndiyo walioanza kupuuza utaratibu huo kwa kuwaagiza wasaidizi wao ndiyo waende kwenye mikutano hiyo.
    Lakini sasa imefikia hata makocha wa timu nyingine tunazoziita ndogo nao wameanza kupuuza mikutano hiyo kwa mfano jana baada ya mechi dhidi ya Yanga, kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime naye alimtuma Msaidizi wake, Ally Jangalu akamuwakilishe.
    Mecky anafanya hivyo kwa sababu tangu anafundidha Mtibwa Sugar ya Morogoro amekuwa akiona makocha Wakuu wa Simba na Yanga hawatokei kwenye mikutano.
    Makocha hawa, Mcameroon Joseph Marius Omog wa Simba, Mzambia George Lwandamina wa Yanga na Mromania Aristica Cioaba wa Azam FC wote wana uzoefu wa kufanya kazi katika mashindano makubwa na wanajua utaratibu wa kuzungumza baada ya mechi.
    Lakini kwa sababu wote walikuja nchini wakakuta makocha Wasaidizi ndiyo wanakwenda kuzungumza baada ya mechi, hawakuona sababu za kuubadilisha utaratibu huo. Mwanzoni mwa utaratibu huu, inakumbukwa wapo makocha walitozwa faini kwa kutotokea kwenye mikutano hiyo.
    Lakini sasa limekuwa jambo la kawaida mikutano hiyo inakuwa ya makocha wasaidizi na ajabu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeonyeshwa kuridhishwa na hilo. 
    Bodi ya Ligi na TFF wanapaswa kuwa mstari mbele kusimamia taratibu walizojiwekea katika uendeshaji wa mashindano na soka ya nchi hii kwa ujumla.
    Ligi Kuu ya nchi hii kwa sasa ni kubwa sana, ina wadhamini na inarushwa moja kwa moja na Televisheni, hivyo lazima ziwepo fursa za kuwafanya wale wanaoipiga jeki ligi hiyo wafurahie.
    Mfaransa Arsene Wenger wa Arsenal na Mourinho wanaelekea kwenye chumba cha mikutano na waandishi wa Habari baada ya kila mechi, lakini Omog na Lwandamina wanawahi kwenye basi la timu. Hii haijatulia.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA NINI MAKOCHA WAKUU WANAKWEPA MIKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top