• HABARI MPYA

  Wednesday, May 10, 2017

  KAGERA SUGAR KUPINGA KADI NYEKUNDU YA MBARAKA JANA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Kagera Sugar leo inatarajiwa kuwasilisha malalamiko Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga kadi nyekundu aliyoonyeshwa mshambuliaji wao, Mbaraka Yussuf Abeid katika mchezo dhidi ya Yanga jana.
  Kagera Sugar ilifungwa 2-1 na wenyeji, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na bahati mbaya mfungaji wa bao lao na mshambuliaji wao tegemeo, Mbaraka Yussuf hakumaliza mechi.
  Refa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Ngole Mwangole wa Mbeya alimtoa nje kwa kadi nyekundu Mbaraka Yussuf Abeid dakika ya 87 baada ya kumchezea rafu beki wa Yanga, Kevin Yondan.
  Mbaraka Yussuf Abeid aliifungia Kagera Sugar jana ikawa 1-1 kabla ya Yanga kupata bao la pili
  Hata hivyo, kipindi cha pili Mbaraka Yussuf akatolewa nje kwa kadi nyekundu

  Lakini akizungumza na Bin Zubery Sport – Online jana, Mratibu wa Kagera Sugar, Mohammed Hussein alisema kwamba wanaandikia barua TFF kupinga kadi hiyo kama ilivyo walivyowahi kufanya Yanga, kupinga kadi ya Obrey Chirwa.
  Alisema mchezaji wao hakucheza rafu zaidi ya kuruka juu tu kiungwana kuwania mpira dhidi ya beki wa Yanga, Yondan. “Yondan pale alimdanganya refa, na refa akadanganyika, lakini naamini wakirudia kuangalia teknolojia ya picha za video wataona vizuri na watabatilisha maamuzi yao,”alisema. 
  Alisema kadi hiyo itamkwamisha Mbaraka katika harakati zake za kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hadi sasa akiwa ana mabao 12, nyuma ya Simon Msuva wa Yanga, anayeongoza kwa mabao yake 13.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAGERA SUGAR KUPINGA KADI NYEKUNDU YA MBARAKA JANA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top