• HABARI MPYA

  Monday, May 01, 2017

  FAINALI KOMBE LA TFF MEI 28…UWANJA KITENDAWILI

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  FAINALI ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayojulikana kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) itafanyika Mei 28, mwaka huu katika Uwanja utakaotajwa baada ya droo maalum itakayofanyika ‘Live’ Azam TV.
  Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema jioni hii mjini Dar es Salaam kwamba, kwa kuwa fainali ya mwaka huu itahusisha timu za mikoa tofauti, Simba ya Dar e Salaam na Mbao FC ya Mwanza, basio itapigwa droo maalum ya kuchagua Uwanja wa kufanyikia mchezo huo.  
  Fainali ya mwaka jana ilizikutanisha timu za Dar es Salaam tupu, Azam na Yanga iliyoibuka bingwa kwa ushindi wa 3-0 hivyo hakukuwa na droo ya kuchagua Uwanja.
  Tayari Yabga imevuliwa taji la ASFC, kufuatia kipigo cha 1-0 kutoka kwa wenyeji, Mbao FC katika mchezo wa Nusu Fainali jana jioni Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. 
  Yanga wenyewe walijifunga bao hilo dakika ya 27, baada ya beki wake, Andrew Vincent ‘Dante’ kuunganishia nyavuni kwake krosi ya Pius Buswita katika harakati za kuokoa.
  Simba yenyewe iliitoa Azam FC katika Nusu Fainali ya kwanza Jumamosi Uwanja wa Taifa kwa ushindi wa 1-0 pia, bao pekee la Mohammed ‘Mo’ Ibrahim kipindi cha pili, mchezaji ambaye hata hivyo hakumaliza mchezo baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: FAINALI KOMBE LA TFF MEI 28…UWANJA KITENDAWILI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top