• HABARI MPYA

    Monday, April 04, 2016

    MALALAMIKO YA STEWART AZAM INAVYOFANYIWA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa mwamuzi wa mchezo wao wa jana dhidi ya Toto Africans, alitakiwa kuahirisha mechi hiyo ndani ya dakika 20 za mwanzo kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jijini Mwanza.
    Azam FC iliweza kuambulia sare ya bao 1-1 kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika  Uwanja wa CCM Kirumba, ambapo mvua hiyo ilianza kunyesha dakika chache kabla ya mechi hiyo kuanza.
    Akizungumza na mwandishi wetu, Hall alisema walikuwa na vita tatu ndani ya mchezo huo, ya kupambana na hali ya uwanja, waamuzi pamoja na wapinzani wao hao, jambo ambalo liliwafanya washindwe kuishinda vita hiyo kwa kuambulia sare.
    Stewart Halll amelalamikia Azam FC kuchezeshwa kwenye mvua jana

    “Ni matokeo mabaya kwa upande wetu, lakini kuna sababu kadhaa zimepelekea hayo kutokea  la kwanza ni sehemu ya kuchezea mpira (pitch), ingekuwa ni mimi mpira usingechezeka, kwangu mimi baada ya dakika 20 ningeahirisha mchezo huo hata kabla ya sisi kupata bao baada ya mistari ya chaki kutoonekana, nilisimama eneo hilo na kuona mwamuzi msaidizi akishindwa kuiona mistari hiyo, hata mwamuzi wa kati naye alishindwa lakini hawakulizingatia hilo, vilevile mpira ulishindwa kuenda chini pale ulipopigwa kutokana na maji kujaa,” alisema.
    Hall alisema baada ya mpira kuendelea ulikuwa ni wa nguvu sawa na kudai kuwa kwa hali ile huwezi kupata mchezaji bora kwani mipango ya timu inashindwa kwenda vizuri, kwani mchezaji huanza kupambana na uwanja kabla ya kufikiria jambo jingine.
    “Wachezaji wangu walishindwa kwenda mbele na mipira kabisa, Sure Boy alishindwa, Farid Mussa alishindwa, Messi (Ramadhan Singano) asingeweza kucheza kwenye hali hii kwani ilikuwa ni ya kupambana sana,” alisema.
    Hali ya Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza jana wakati wa mchezo wa Azam na wenyeji, Toto Africans

    Waamuzi wachovu
    Kocha huyo, 60, alisema kuwa kwa mara nyingine amesikitishwa na kiwango cha waamuzi kutoka Tanzania kutokana na kuwaumiza mno kwa maamuzi ya kushangaza ndani ya mchezo huo.
    “Waamuzi walishindwa kutenda haki, mara nyingi tulipokuwa tukishambulia alipiga filimbi ya kuotea (offside) au tumefanya madhambi, Wanga aliangushwa ndani ya eneo la 18 lakini hatuupewa penalti, ilikuwa ni ngumu sana kushinda vita tatu tulizokuwa tukipigana ndani ya mchezo, kwanza kupambana na uwanja, pili waamuzi na tatu Toto African.
    “Vita tatu ni nyingi sana, vita moja au mbili ni rahisi kupambana lakini tatu ndani ya mchezo mmoja ni nyingi sana, Toto Africans ilipoteza sana muda kipindi cha pili takribani dakika 11, lakini mwamuzi aliongeza dakika tatu tu, hata nilipojaribu kumwambia alibakia kucheza tu na hili linaonyesha kuwa kuna kitu walikuwa wakitafuta,” alisema.
    Wachezaji wa Azam FC wakifanya mazoezi jana Uwanja wa CCM Kirumba kabla ya mechi na Toto

    Ndanda itaturudisha  
    Kocha huyo raia wa Uingereza alisema kuwa mchezo ujao wa keshokutwa Jumatano (Aprili 6) dhidi ya Ndanda ndani ya Uwanja wa Azam Complex unatarajia kuwarejesha kwenye hali yao ya kawaida huku akidai kuwa ni lazima washinde mchezo huo.
    “Utakuwa ni mchezo mgumu kwani tunajua kuna baadhi ya watu wataipa fedha Ndanda ili iweze kutuzuia sisi kwa kucheza soka la kujilinda zaidi, hivyo sisi tumejipanga na tunajua namna ya kuzuia mbinu zao hizo,” alisema.
    Azam FC inayodhaminiwa na Benki bora kabisa nchini ya NMB, kwa sasa imejikusanyia jumla ya pointi 51 katika nafasi ya tatu, nyuma ya Yanga iliyojikusanyia 53 huku Simba iliyocheza michezo miwili zaidi dhidi ya timu hizo ikiwa kileleni kwa pointi 57.
    Tayari kikosi cha Azam FC kimerejea Dar es Salaam leo asubuhi kwa ndege ya Shirika la Fastjet ikiokea jijini Mwanza, ambapo kesho saa 2.30 asubuhi kitafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuivaa Ndanda.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALALAMIKO YA STEWART AZAM INAVYOFANYIWA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top