• HABARI MPYA

  Saturday, August 03, 2019

  MOLINGA ‘FALCAO’ ASAINI KWA MKOPO WA MWAKA MMOJA YANGA SC, KINDOKI ATEMWA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI David Molinga ‘Falcao’ amesaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na Yanga SC ya Dar es Salaam kwa mkopo akitokea AC Lega ya kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).  
  Baada ya kusajiliwa kwa Molinga ‘Falcao’, Mkongo mwenzake, kipa Klaus Kindoki ameruhusiwa kuondoka ili Yanga ibaki na wachezaji 10 wa kigeni kwa mujibu wa kanuni.
  Wachezaji wengine wa kigeni Yanga SC ni Nahodha Papy Kabamba Tshishimbi pia kutoka DRC, kipa Mkenya Farouk, Sadney Urikhob kutoka Namibia, Lamine Moro kutoka Ghana, Juma Balinya kutoka Uganda, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana wote wa Rwanda, Mustapha Seleman kutoka Burundi na Maybin Kalengo kutoka Zambia.
  Kwa ujumla Yanga SC imeimarisha kikosi chake msimu huu kwa kusajili nyota wengine sita wapya, kipa Metacha Mnata kutoka Mbao FC alikokuwa anacheza kwa mkopo kuoka Azam FC, mabeki Muharami Salum Issa ‘Marcelo’ kutoka Malindi ya kwao, Zanzibar, Ally Mtoni 'Sonso' kutoka Lipuli FC, Ally Ally kutoka KMC ya Kinondoni, viungo wa ulinzi, Abdulaziz Makame kutoka Mafunzo ya Zanzibar na Mapinduzi Balama kutoka Alliance FC ya Mwanza.
  Wakati huo huo, kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi yake leo mjini Morogoro katika kambi yake ya kujiandaa na msimu mpya baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Friends Rangers jana, mabao ya mshambuliaji wake mpya kutoka Namibia, Sadney Urikhob dakika ya 38 na Nahodha mpya, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi.
  Yanga SC watamenyana na Kariobangi Sharks ya Kenya Jumapili Uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam katika kilele cha Wiki ya Mwananchi.
  Ikiwa kambini mjini Morogoro, Yanga imecheza mechi nne za kujipima nguvu na kushinda zote, 10-1 dhidi ya dhidi ya Tanzanite, 7-0 dhidi ya ATN, 2-0 dhidi ya Moro Kids na 1-0 dhidi ya Mawenzi Market.
  Na yote hayo ni maandalizi ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga SC wakianza na Township Rollers ya Botswana kati ya Agosti 9 na 11 mjini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao mjini Gaborone kati ya Agosti 23 na 25.
  Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza Yanga itakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MOLINGA ‘FALCAO’ ASAINI KWA MKOPO WA MWAKA MMOJA YANGA SC, KINDOKI ATEMWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top