• HABARI MPYA

    Saturday, August 24, 2019

    AZAM FC YAWAPIGA FASIL KENEMA 3-1 NA KUSONGA MBELE KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA

    Na Saada Salim, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Azam FC imefanikiwa kuingia Raundi ya Pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Fasil Kenema jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
    Kwa matokeo hayo, Azam FC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza nchini Ethiopia na sasa itamenyana na Triangle United ya Zimbabwe iliyoitoa Rukinzo ya Burundi.
    Mabao ya Azam FC katika mchezo wa leo yamefungwa na mchezaji mpya kutoka Ivory Coast, Richard Ella Djodi mawili na mshambuliaji mwenzake, Obrey Chirwa, wakati la Fasil Kenema limefungwa na Mujib Kasim.

    Djodi alifunga bao la kwanza dakika ya 23 kwa shuti la kiufundi baada ya kumgeuza beki wa Kenema kufuatia pasi nzuri ya kiungo mjuvi Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na la pili dakika ya 31 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya yeye mwenyewe kuchezewa rafu nje kidogo ya eneo la hatari.
    Kenema wakapata bao lao pekee dakika ya 36 kupitia kwa Mujib Kasim aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Surafel Dagnachew kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Shemekit Gugesa aliyewachachafya mabeki wa Azam.
    Mzambia Chirwa akaihakikishia Azam FC nafasi ya kusonga mbele baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 58 alimalizia mpira uliorudi baada ya kugonga nguzo kufuatia shuti kali la kiungo mshambuliaji Iddi Suleiman 'Nado' aliyefanikiwa kwanza kuwapangua mabeki wa Kenem.
    Kwenye Raundi ya pili, Azam FC wataanzia nyumbani tena kati ya Septemba 13 na 15, kabla ya kusafiri kwenda Zimbabwe kwa mchezo wa marudiano kati ya Septemba 27 na 29.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa: Razak Abalora, Frank Domayo, Nico Wadada, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Yakubu Mohammed, Emmanuel Mvuyekure, Salum Abubakar, Obrey Chirwa/Donald Ngoma dk 80, Richard Ela Djodi/Abdallah Masoud ‘Cabaye’dk64 Na Idd Suleiman ‘Nado’/Iddy Kipagwile dk70.
    Fasil Kenema: Samake Mickel, Coulibaly Yarefo, Surafel Dagnachew, Azuk Ibob/Yosef Tekeleargawi dk77, Solomon Habte, Saed Hassen/ Alembrehane Azanawe dk46, Enyew Kassahum dk46, Habtamu Tekeset, Yared bayeh, Shemekit Gugesa, Amsalu Telahun na Mujib Kasim.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAWAPIGA FASIL KENEMA 3-1 NA KUSONGA MBELE KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top