• HABARI MPYA

    Monday, August 12, 2019

    YANGA SC WAENDA KAMBINI MOSHI KUJIANDAA KWA MARUDIANO NA TOWNSHIP ROLLERS

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Yanga SC kitaondoka kesho Dar es Salaam kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Township Rollers Agosti 24 Uwanja wa Taifa mjini Gaborone.
    Kocha Mkongo, Mwinyi Zahera alihitaji kambi katika mji wenye hali ya hewa ya baridi sawa na Gaborone na uongozi umeamua kuipeleka timu Moshi ambako ikiwa huko itacheza pia mechi mbili za kujipima nguvu.
    Yanga SC inahitaji ushindi wa ugenini lazima ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo, kufuatia kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 nyumbani, Jumamosi na Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Siku hiyo, Yanga SC ilitanguliwa kwa bao la dakika ya saba tu lililofungwa na Phenyo Serameng, kabla ya kiungo Mnyarwanda, Patrick Sibomana kuisawazishia ‘Timu ya Wananchi’ dakika ya 86. 
    Serameng alifunga bao lake baada ya kumpindua beki wa kushoto wa Yanga SC, Muharami Issa ‘Marcelo’ kufuatia pasi ya Kanogelo Matsabu na kufumua shuti la kiufundi kwa mguu wake wa kushoto kumtungua kipa mpya, Metacha Boniphace Mnata aliyesajiliwa kutoka Mbao FC ya Mwanza.
    Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Sibomana alipoteza nafasi ya kuifungia bao Yanga SC dakika ya 30 baada ya mkwaju wake wa penalti kupanguliwa na kipa Wagarre Dikago.
    Penalti hiyo ilitolewa na refa George Gatpgato kutoka Burundi baada ya mpira uliopigwa na kiungo Mapinduzi Balama kumgonga beki wa Township Rollers, Ofentse Nato kwenye boksi. 
    Ofentse Nato tena akaunawa mpira kwenye boksi alioruka kichwa cha mkizi kuokoa krosi ya Issa Bigirimana kutoka upande wa kulia na Sibomana akaenda kuifungia Yanga bao la kusawazisha dakika ya 86.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAENDA KAMBINI MOSHI KUJIANDAA KWA MARUDIANO NA TOWNSHIP ROLLERS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top