• HABARI MPYA

  Saturday, August 03, 2019

  SIMBA SC YAINGIA MKATABA NA BENKI YA EQUITY KUTOA KADI MPYA ZA WANACHAMA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba SC imeingia mkataba na benki ya Equity kwa ajili kusimamia mradi wa kadi mpya za wanachama na mashabiki ambazo zitajulikana kama Simba Card.
  Taarifa ya Simba SC imesema kwamba kadi hizo zitatumiwa na wanachama na mashabiki kuweka akiba ye pesa na kutoa pindi wanapotaka kutumia, lakini pia kulipa ada ya kila mwaka, kununua tiketi za kuingia mpirani, na kupata punguzo la mpaka 10% kwenye maduka makubwa ambayo tutashirikiana nayo.
  Faida kubwa kwa klabu katika kadi hizo ni makato yanayopatikana wakati wa kufungua akaunti, kukusanya ada kisasa na mara moja kwa mwaka, na kupata takwimu sahihi za mashabiki iwapo kila shabiki atafungua akaunti.

  Kadi hizo zitaanza kutolewa Septemba mosi mwaka huu kwa kuwabadilishia kadi wanachama wa sasa na baadae litaendelea kwa wanachama wapya na mashabiki. 
  Wakati huo huo, kikosi cha Simba SC kinaendelea na mazoezi yao Uwanja wa Boko Veterani kuelekea mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Power Dynamos Jumanne mjini Dar es Salaam katika tamasha la Simba Day.
  Simba ilirejea Dar es Salaam juzi baada ya kambi ya zaidi ya wiki tatu mjini Rusternburg, Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya.
  Na ikiwa huko ilipata mechi nne za kujipima nguvu, ikishinda mbili na kutoa sare mbili. Ilishinda 4-1 dhidi ya Orbit Tvet, 4-0 dhidi ya Platnums Stars kabla ya sare mbili mfululizo za 1-1 dhidi ya Township Rollers ya Botswana na Orlando Pirates ya Johannesburg.
  Simba SC imelazimika kurudisha nyuma kwa siku mbili tamasha hilo ambalo kila mwaka hufanyika Agosti 8 baada ya ratiba ya Ligi Mabingwa Afrika kutoka ikionyesha mechi za kwanza za raundi ya Kwanza zitachezwa kati ya Agosti 9 na 11. 
  Simba SC wataanzia ugenini dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji kati ya Agosti 9 na 11 kabla ya kurejea nyumbani kwa mchezo wa marudiano kati ya Agosti 23 na 25.
  Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza, Simba itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi na ikifuzu mtihani huo pia itaingia tena hatua ya makundi.
  Wakati Simba ni mabingwa wa Bara, Power Dynamos walimaliza nafasi ya sita kwenye Kundi B Ligi Kuu ya Zambia msimu uliopita, ambalo Green Eagles iliongoza na kuingia fainali na kufungwa kwa penalti 3-1 na ZESCO United walioibuka mabingwa wa Zambia baada ya sare ya 0-0.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAINGIA MKATABA NA BENKI YA EQUITY KUTOA KADI MPYA ZA WANACHAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top