• HABARI MPYA

    Tuesday, August 20, 2019

    KIMANZI KOCHA MKUU TENA HARAMBEE STARS BAADA YA MFARANSA KUFUKUZWA

    KOCHA Francis Kimanzi amerejea kufundisha timu ya taifa ya Kenya akichukua nafasi ya Mfaransa, Sebastien Migne  aliyefukuzwa Harambee Stars wiki iliyopita.
    Hiyo inafuatia Harambee Stars kutolewa na Tanzania 'Taifa Stars' katika Raundi ya kwanza ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwakani nchini Cameroon kwa penalti baada ya sare ya jumla ya 0-0.
    Kimanzi aliyekuwa Msaidizi wa Migne kwa miezi 15 iliyopita Harambee Stars ametambulishwa rasmi leo kupewa Ukocha Mkuu wa timu yake ya taifa. 
    Kimanzi anakumbukwa kwa kazi yake nzuri iliyosaidia kuinua Kenya kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hadi nafasi ya 68 mwaka 2008.
    Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Nick Mwendwa amesema kwamba Kimanzi atapewa ushirikiano wa kutosha baada ya kupewa mikoba ya Migne.

    Francis Kimanzi amerejea Harambee Stars kuchukua nafasi ya Mfaransa, Sebastien Migne aliyefukuzwa 

    Na tayari Kimanzi ameteua benchi lake la Ufundi na atakuwa anasaidiwa na kocha na beki wa zamani wa Gor Mahia, Zedekiah Otieno ambaye naye amewahi kuwa kocha wa Harambee Stars mwaka 2011.
    Michael Igendia atabakia kuwa kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili akisaidiwa na Enos Karani, wakati Lawrence Webo aliyekuwa na timu ya taifa ya wanawake kwenye mechi za kufuzu Kombe la Mataifa yav Afrika ameteuliwa kuwa kocha wa makipa.
    Mtihani wa kwanza wa benchi jipya la Ufundi utakuwa Septemba 8 wakati Kenya itakapomenyana na Uganda, The Cranes katika mchezo wa kirafiki mjini Nairobi kabla ya kusafiri kwenda Morocco au Tunisia kumenyana na Libya Oktoba 11 huku FKF ikitafuta mechi nyingine ya kirafiki itakayofanyika Oktoba 15.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIMANZI KOCHA MKUU TENA HARAMBEE STARS BAADA YA MFARANSA KUFUKUZWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top