• HABARI MPYA

  Monday, August 13, 2018

  YANGA SC YAENDELEZA UBABE MECHI ZA KIRAFIKI MORO, YAICHAPA KOMBAINI YA KILOSA 1-0

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  YANGA imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kujipima nguvu baada ya leo pia kushinda 1-0 dhidi ya wenyeji, Kombaini ya Kilosa.
  Bao pekee la Yanga leo limefungwa na beki wa kushoto Simon Gustavo dakika 32 akimalizia krosi ya Paul Godfrey, kiungo aliyechezeshwa beki ya kulia leo. 
  Kocha Mkongo, Mwinyi Zahera leo aliwapanga wachezaji wengi ambao hawakucheza mechi ya jana dhidi ya Mawezi Market na kikosi kilirejea Morogoro mjini baada ya mechi hiyo kuendelea na kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya USM Alger Jumapili. 
  Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Yanga, baada ya jana kuilaza Mawenzi Market 1-0 pia, bao pekee la mshambuliaji mpya, Haritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Mchezo wa leo ulikuwa maalum wa kumuaga aliyekuwa Nahodha wa klabu kwa muda mrefu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye baada ya kuitumikia klabu tangu mwaka 2006, sasa anakuwa Meneja wa timu.
  Cannavaro alicheza kwa dakika 10 tu kabla ya mchezo kusimama kumpa fursa ya kuaga na kukabidhi beji kwa Nahodha mpya, Kelvin Yondan na jezi yake, namba 23 kwa Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
  Na leo Kilosa Cannavaro alipata fursa ya kuwaaga mashabiki wa timu hiyo, kwa kupiga nao picha na kufurahi nao kabla ya mechi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAENDELEZA UBABE MECHI ZA KIRAFIKI MORO, YAICHAPA KOMBAINI YA KILOSA 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top