• HABARI MPYA

  Wednesday, August 01, 2018

  SALAMBA AWEKA REKODI YA KUFUNGA BAO LA KWANZA LA MSIMU SIMBA SC IKITOKA SARE 1-1 NA WAARABU UTURUKI

  Na Mwandishi Wetu, ISTANBUL
  MSHAMBULIAJI mpya, Adam Salamba ameweka rekodi ya kufunga bao la kwanza la msimu wa 2018-2019 la Simba SC akiwasawazishia Wekundu wa Msimbazi katika sare ya 1-1 na Mouloudia Club of Oujda ya Uwanja wa Kartepe Green Park mjini Istanbul.
  Salamba aliyesajiliwa Mei mwaka huu kutoka Lipuli ya Iringa, alifunga bao hilo kipindi cha pili baada ya kuwa sehemu ya wachezaji wote wa Simba SC walioingia kipindi hicho kuwabadili wenzao walioanza, likiwa la kusawazisha baada ya MC Oujda inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kama Botola kutangulia.
  Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa mabingwa hao wa Tanzania, Simba SC katika kambi ya Uturuki walipowasili Julai 22 kujiandaa na msimu mpya.

  Adam Salamba (kushoto) ameisawazishia Simba katika sare ya 1-1 na MC Oujda leo mjini Istanbul

  Kikosi cha Simba SC kilichoanza kwenye mechi ya leo dhidi ya MC Oujder

  Na unakuwa mchezo wa kwanza kabisa kwa kocha mpya, Mbelgiji Patrick J Aussems anayesaidiwa na Mrundi, Masoud Juma, Mtunisia Adel Zrena Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili na Muharami Mohammed ‘Shilton’ kocha wa makipa na wa kwanza wa msimu pia.
  Kikosi cha Simba SC kilichoweka kambi katika hoteli ya Reen Park & Resorts mjini Istanbul, kikifanya mazoezi yake katika moja ya viwanja saba vilivyoizunguka hoteli hiyo, kinatarajiwa kurejea nchini Agosti 6 tayari kwa tamasha la kila mwaka la klabu, Simba Day ambalo hufanyika Agosti 8 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Na siku hiyo, Simba SC itamenyana na mabingwa mara mbili wa Afrika, Asante Kotoko ya Ghana  waliobeba taji hilo enzi za Klabu Bingwa Afrika katika miaka ya 1970 na 1983. Katika safari yao la kulifuata taji la 1970, Kotoko walikutana na wapinzani wa jadi wa Simba SC, Yanga kwenye Robo Fainali na kuitoa kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya sare ya 1-1 Dar es Salaam na ushindi wa 2-0 mjini Kumasi.
  Vikosi vya Simba SC leo vilikuwa; Kipindi cha kwanza; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Asante Kwasi, James Kotei, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Shiza kichuya, Cletus Chama, Meddie Kagere, Hassan Dilunga na Emmanuel Okwi.
  Kipindi cha pili;  Deo Munishi ‘Dida’, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili, Paul Bukaba, Muzamil Yassin, Marcel Kaheza, Said Ndemla, Adam Salamba, Mohammed Rashid na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SALAMBA AWEKA REKODI YA KUFUNGA BAO LA KWANZA LA MSIMU SIMBA SC IKITOKA SARE 1-1 NA WAARABU UTURUKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top