• HABARI MPYA

  Wednesday, August 01, 2018

  KOCHA MPYA TAIFA STARS KUWASILI AGOSTI…AMEKWISHAANZA KAZI YA KUUNDA KIKOSI CHA KUIVAA UGANDA SEPTEMBA 8 KAMPALA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA mpya wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars anatarajiwa kuwasili nchini mapema Agosti kwa ajili ya kusaini mkataba na kuanza kazi mara moja.
  Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba anakuja kocha mkubwa sana wa kigeni, ambaye akifika Watanzania watampenda.
  “Mwalimu amekwishaanza kazi, amekwishaanza kufuatilia wachezaji wetu, kwa hivyo mambo yanakwenda vizuri, benchi la Ufundi la hapa nyumbani limekwishaanza kufanya kazi na mwalimu, lakini hatuwezi tukamtangaza mwalimu kwa sababu kuna mambo madogo madogo ya ndani ambayo lazima tuyamalize sisi na yeye,”amesema Kidau.
  Na mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Milambo ya Tabora, Simba SC, Vijana ‘Kabakayeka’ za Dar es Salaam amesema kwamba kocha huyo mpya atafanya kazi na waliokuwa wasaidizi wa kocha Yanga.

  Kikosi cha Taifa Stars kilichoifunga DRC 2-0 Machi 27, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam

  Baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Taifa Stars itasafiri kuwafuata Uganda kwa mechi ya Septemba 8, mwaka huu kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
  Lakini kwa miezi minne sasa Taifa Stars haina kocha baada ya kumaliza mkataba kwa Salum Mayanga, ambaye aliiongoza timu kwa mara ya mwisho Machi 27, mwaka huu ikishinda 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Wafungaji wa mabao hayo walikuwa, Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Shiza Ramadhani Kichuya wa Simba ya nyumbani yanayoipa ushindi wa kwanza Tanzania tangu Julai 7 mwaka jana ilipoichapa kwa matuta Lesotho baada ya sare ya 0-0 kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
  Katika hatua nyingine, Kidau amezungumzia mafanikio ya timu ya wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens akisema kwamba wachezaji wote wamefunguliwa akaunti benki ya Biashara ya Kenya (KCB) ambazo wataingizwa fedha zao za zawadi na malimbikizo ya posho zao.
  Hiyo ni baada ya malalamiko ya baadhi ya wachezaji kwamba baada ya ushindi wao wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge wiki iliyopita wameambulia kupewa Sh. 150,000 kila mmoja, mbali ya Sh. 200,000 walizopewa kila mmoja kama posho za kambi ya maandalizi mjini Dar es Salaam.
  Pamoja na kufanikiwa kutetea Kombe la CECAFA Challenge baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Ethiopia Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali, Rwanda Ijumaa iliyopita, lakini Kilimanjaro Queens walirejea nyumbani kwa basi, jambo ambalo limewasikitisha wapenzi wengi wa soka.
  Ushindi wa Ijumaa uliifanya Kilimanjaro Queens kumaliza na pointi saba sawa na Uganda, baada ya kushinda mechi mbili, sare moja na kufungwa moja lakini wastani wao mzuri wa mabao unawapa taji la pili mfululizo la CECAFA Challenge. 
  Ethiopia imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake sita, wakati Kenya imekuwa ya nne kwa pointi zake nne sawa na wenyeji, Rwanda walioshika mkia. Pamoja na kuburuza mkia, lakini Rwanda ndiyo timu pekee iliyowafunga mabingwa Tanzania Bara, 1-0 katika mchezo wa kwanza kabisa.
  Mwaka 2016 michuano hiyo ilifanyika kwa mtindo wa makundi, baadaye mtoano kuanzia Nusu Fainali wakati mwaka huu mashindano yamechezwa kwa mtindo wa Ligi, na bingwa ameamuliwa kwa pointi nyingi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA MPYA TAIFA STARS KUWASILI AGOSTI…AMEKWISHAANZA KAZI YA KUUNDA KIKOSI CHA KUIVAA UGANDA SEPTEMBA 8 KAMPALA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top