• HABARI MPYA

    Sunday, August 12, 2018

    DANNY LYANGA AFUNGA AZAM FC YATOA SARE 1-1 NA EXPRESS UGANDA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo imeendelea na mechi za kujiweka sawa na msimu ujao ikiwa kambini nchini Uganda, safari hii ikitoka sare ya bao 1-1 na Express.
    Mchezo huo uliokuwa mkali na wa aina yake, ulifanyika Uwanja wa Mutesa II, ikiwa ni mechi ya tatu ya kirafiki kwa mabingwa hao kambini nchini humo.
    Mechi mbili za awali, Azam FC ilitoka suluhu na URA kabla ya kupoteza kwa kufungwa mabao 4-2 dhidi ya washindi wa pili wa Ligi Kuu Uganda, KCCA.
    Azam FC ndio iliyoanza kuliona lango la wapinzani wake kwa bao safi lililofungwa na Danny Lyanga dakika ya 15 akiinyanyua mpira ‘chop’ uliomshinda kipa wa Express, Mutombora Fabian, akimalizia pasi safi ya juu ya kiungo, Mudathir Yahya.

    Dakika ya 32 Azam FC ilitengeneza nafasi nyingine nzuri, baada ya Lyanga na Tafadzwa Kutinyu kugongeana vema lakini pasi ya mwisho ya Mzimbabwe huyo inakosa mmaliziaji na mpira kuokolewa na mabeki wa Express.
    Azam FC ililazimika kufanya mabadiliko dakika nne baadaye kufuatia kuumia kwa Lyanga na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji Ditram Nchimbi. Hata hivyo ilishuhudiwa bao hilo likidumu hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza.
    Benchi la ufundi la Azam FC chini ya Hans Van Der Pluijm, lilitumia dakika 14 za mwanzo za kipindi cha pili kufanya mabadiliko ya wachezaji watatu kwa dakika tofauti wakiingia beki David Mwantika, washambuliaji Yahya Zayd na Wazir Junior.
    Dakika ya 60 Express ilikuja juu na kufanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Matovu Ruben.
    Azam FC iliendelea kulisakama lango la Express ili kujipatia mabao ya ushindi, ambapo kuelekea dakika 20 za mwisho za mchezo huo ilipoteza nafasi muhimu kupitia kwa Kutinyu na Nchimbi.
    Huo ndio ulikuwa mchezo wa mwisho wa kirafiki kwa Azam FC nchini humo, ambapo itaendelea mazoezi ya kawaida kwa siku tatu zilizobakia kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam Agosti 16 mwaka huu.
    Kikosi cha Azam FC; Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri/Mwantika 50’, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya/Junior 59’, Joseph Mahundi/Zayd 57’, Frank Domayo/Hoza 65’, Danny Lyanga/Nchimbi 36’, Tafadzwa Kut inyu, Ramadhan Singano/Mbaraka 77’
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DANNY LYANGA AFUNGA AZAM FC YATOA SARE 1-1 NA EXPRESS UGANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top