• HABARI MPYA

    Monday, March 19, 2018

    KARIA: TUMEMCHUKULIA HATUA WAMBURA BAADA YA UKAGUZI WA FIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kwamba yanayotokea kwa sasa ndani ya shirikisho hilo ni miongoni mwa matokeo ya utekelezaji wa taarifa za timu ya uchunguzi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Karia ameyasema hayo leo katika mkutano na Wahariri wa vyombo vya Habari hoteli ya SeaScape, Kunduchi mjini Dar es Salaam kuhusu mwenendo mzima na hali halisi ndano ya TFF.
    Na Karia anayasema haya wakati ambao, Makamu wake wa Rais, Michael Richard Wambura amefungiwa na Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo maisha kujihusisha na soka kwa makosa matatu, ambayo ni kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kughushi barua na kushusha hadhi ya TFF.
    Rais wa TFF, Wallace Karia (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu, Wilfred Kidau

    “FIFA walituma Timu ya Uchunguzi kuangalia yale yote yaliyofanyika tangu mwaka 2013 hadi mwaka 2017. Timu ilikaa nchini kwa takribani wiki mbili ikifanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Katibu Mkuu. Yaliyogundulika yameacha doa kubwa na walitoa ripoti na maelekezo ya mambo ya kuyafanyia kazi na ya kuchukulia hatua,”amesema Karia.
    Amesema masharti yote haya yaliambatana na kuzuiwa kwa fedha zetu za miradi nia na wenzao wachache, lakini pia TFF wamekosa fedha za ruzuku kutoka FIFA, dola za Kimarekani Sh. Milioni 3 walizopaswa kulipwa tangu mwaka 2015 hadi 2018.
    “Karibu nchi zote duniani zimenufaika kwa kupata fedha hizi, isipokuwa Tanzania. Kuhakikisha tunatekeleza masharti ya FIFA, hivyo tulipopata ripoti tumeamua kutekeleza kwa asilimia mia moja maagizo yote ya FIFA,”amesema. 
    Rais huyo wa TFF amesema kwamba jambo hilo limepitia hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu zinazohusiana na taarifa za ukaguzi na wahusika wameshirikishwa ipasavyo na utetezi wao ulipeleka kwenye Kamati husika ya Ukaguzi miezi michache iliyopita baada ya kutakiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu.
    “Niseme tu unaposafisha taasisi kuna gharama zake, TFF inahitaji kuungwa mkono zaidi kwa hatua Madhubuti inazochukua za kujisafisha na kusonga mbele. Katika vita hii ya kupambana na udhalimu kwenye mpira wetu hatutarudi nyuma. Tutapambana bila hofu wala woga, ili mradi hakuna dhuluma wala uonevu wala upendeleo kwa yeyote. Na Nitoe wito kama kuna kiongozi au mdau yeyote anayejua ana fedha za TFF kinyume cha utaratibu ajisalimishe mwenyewe,”amesema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA: TUMEMCHUKULIA HATUA WAMBURA BAADA YA UKAGUZI WA FIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top