• HABARI MPYA

    Monday, March 19, 2018

    MANDAWA, CHILUNDA WAONGEZWA TAIFA STARS, BOCCO, ULIMWENGU NA FARID MUSSA WATEMWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga ameongeza wachezaji watatu kwenye kikosi kinachosafiri jioni hii kwenda Algeria, akiwemo mshambuliaji Rashid Mandawa anayecheza BDF ya Botswana.
    Hiyo ni baada ya Mayanga kuwaacha wachezaji wanne wakiwemo washambuliaji wawili, John Raphael Bocco wa Simba SC na Thomas Emmanuel Ulimwengu anayefanya mipango ya kuhamia Bosnia.
    Bocco ameachwa kwa sababu ni majeruhi wakati Ulimwengu imeelezwa kwamba bado anashughulikia mipango ya kucheza Bosnia akitokea Sweden alipokuwa anacheza mara ya mwisho, hivyo ameshindwa kuja kujiunga na Taifa Stars kwa sasa.
    Shaaban Iddi (katikati) na Yahya Zayed sasa wanapatikana Taifa Stars, kasoro Iddi Kipwagile tu (kulia)

    Wengine waliotemwa ni viungo Farid Mussa wa Teneriffe B ya Hispania ambaye imedaiwa klabu yake imemzuia na Hamisi Abdallah wa AFC Leopard ya Kenya ambaye Mayanga amesema tu kwa sababu za kiufungo.
    Wengine walioongezwa kikosini ni wachezaji wa Azam FC, kiungo na nahodha Msaidizi, Himid Mao na mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda ambao wote walikuwa majeruhi ila kwa sasa wameimarika. 
    Taifa Stars inaondoka muda huu kwenda Algeria, ambako watapokewa na Mratibu wa timu, Ahmed Iddi ‘Msafiri’ Mgoyi ambaye mapema leo amewapokea wachezaji wa Simba SC waliokuwa na timu yao Misri, kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe na Erasto Nyoni na viungo Said Ndemla na Shiza Kichuya. 
    Kikosi kamili cha Taifa Stars ni; Makipa; Aishi Manula (Simba SC), Abdulrahman Mohammed (JKU), Ramadhan Kabwili (Yanga SC), mabeki; Shomary Kapombe (Simba SC), Hassan Kessy (Yanga SC), Gardiel Michael (Yanga SC), Kelvin Yondan (Yanga SC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Erasto Nyoni (Simba SC).
    Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Mudathir Yahya (Singida United), Said Ndemla (Simba SC), Faisal Salum (JKU), Abdulaziz Makame (Taifa Jangombe), Ibrahim Ajib (Yanga SC), Shiza Kichuya (Simba SC) na Mohammed Issa ‘Banka’ (Mtibwa Sugar).
    Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Simon Msuva (Difaa Hassan El Jadida/Morocco), Rashid Mandawa (BDF/Botswana), Shaaban Iddi na Yahya Zayed (Azam FC)
    Kocha Mkuu ni Salum Mayanga, Msaidizi wake, Patrick Mwangata, Mtunza Vifaa; Ally Ruvu, Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya na Meneja Daniel Msangi. 
    Taifa Stars itamenyana na wenyeji Algeria, The Greens Alhamisi katika mchezo wa kirafiki, kabla ya kurejea nyumbani kucheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), The Leopards Machi 27 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Mara ya mwisho Taifa Stars iliteremka uwanjani Novemba 1 mwaka jana na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Benin katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou wenyeji wakitangulia kwa bao Nahodha, Stephane Sessegnon aliyefunga kwa penalti dakika ya 33 kabla ya mshambuliaji wa zamani wa Simba na Dhofar SC ya Oman, Elias Maguri kuisawazishia Tanzania dakika ya 50.
    Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 146 kwenye viwango vya FIFA, wakati DRC ni ya 39 na Algeria ni ya 60.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANDAWA, CHILUNDA WAONGEZWA TAIFA STARS, BOCCO, ULIMWENGU NA FARID MUSSA WATEMWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top