• HABARI MPYA

  Friday, February 09, 2018

  YANGA YAZUIWA KUFANYA MAZOEZI UWANJA WA TAIFA KUELEKEA MECHI YAKE YA UFUNGUZI LIGI YA MABINGWA JUMAMOSI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC Alhamisi jioni wamezuiwa kufanya mazoezi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kuelekea mchezo wa kwanza wa Raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Saint Louis FC ya Shelisheli Jumamosi.
  Kwa mujibu wa habari kutoka Yanga ni kwamba uongozi wa Uwanja wa Taifa umewazuia kufanya mazoezi kwa kuhofia utaharibika eneo la kuchezea na kwa sababu wikiendi hii kutakuwa na mechi mbili mfululizo za michuano ya Afrika.
  Na si zuio hilo haliihusu Yanga pekee, bali hata wapinzani wao wa jadi, Simba SC ambao nao Jumapili watamenyana na Gendarmerie Tnale ya Djobouti katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
  Uongozi wa Uwanja wa Taifa umesema kwa kuwa nyasi za Uwanja huo zimeoteshwa hivi karibuni, bado haziwezi kuhimili mikiki mfululizo ya mechi.
  Mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa anatarajiwa kuendelea kuibeba Yanga hadi kwenye michuano ya Afrika pia
  Kwa sababu hiyo zaidi ya mechi hizo za kwanza za Raundi ya Kwanza ya michuano ya Afrika Jumamosi na Jumapili ni wageni tu, Saint Louis FC na Gendarmerie Tnale wataruhusiwa kufanya mazoezi Ijumaa na Jumamosi.
  Saint Louis FC watafanya mazoezi kesho jioni wakati Gendarmerie Tnale wanaweza kufanya Jumamosi asubuhi au mchana na kuna uwezekano pia Simba SC wakaruhusiwa kufanya mazoesi usiku wa Jumamosi.
  Baada ya kuzuiwa kufanya mazoezi leo Uwanja wa Taifa, Yanga walikwenda kufanya Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi Tanzania, kilichopo Kurasini mjini Dar es Salaam, wakati kesho watafanya Uwanja wa Gymkhana.  
  Mchezo kati ya Yanga na Saint Louis FC utachezeshwa na marefa Belay Tadesse Asserese atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera Tigle Gizaw Belachew na Kinfe Yilma Kinfe wote kutoka Ethiopia sawa na refa wa akiba, Amanuel Heleselass Worku wakati Kamishna Frans Vatileni Mbidi anatokea Namibia.
  Mechi ya marudiano kati ya Februari 20 na 21 itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar na kamishna atatoka Mauritius.  Mwamuzi wa kati atakuwa Andofetra Avombitana Rakotojaona akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Lionel Hasinjarasoa Andrianantenaina na mwamuzi msaidizi namba mbili Pierre Jean Eric Andrivoavonjy na mwamuzi wa akiba Hamada el Moussa Nampiandraza, kamishna wa mchezo huo Ahmad Nazeer Hossen Bowud.
  Mechi kati ya Simba na Gendarmerie Tnale itachezeshwa na refa Alier Michael James atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Abdallah Suleiman Gassim, Gasim Madir Dehiya washika vibendera, Kalisto Gumesi mezani na Kamishna Mmonwagotlhe Edwin Senai kutoka Botswana.
  Mchezo wa marudiano utakaochezwa Djibouti kati ya Februari 20 na 21,2018 wenyewe utachezeshwa na waamuzi kutoka Burundi na Kamishna wa mchezo atatokea nchini Rwanda.
  Mwamuzi wa kati ni Eric Manirakiza akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Pascal Ndimunzigo,mwamuzi msaidizi namba mbili Willy Habimana,mwamuzi wa akiba Pacifique Ndabihawenimana na kamishna Gaspard Kayijuka.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAZUIWA KUFANYA MAZOEZI UWANJA WA TAIFA KUELEKEA MECHI YAKE YA UFUNGUZI LIGI YA MABINGWA JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top