• HABARI MPYA

  Thursday, February 01, 2018

  YANGA YAONDOKA LEO MBEYA KUIFUATA LIPULI LIGI KUU JUMAMOSI

  Na David Nyembe, MBEYA
  KIKOSI cha Yanga kinaondoka leo mjini Mbeya kwenda Iringa tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Lipuli Uwanja Samora Jumamosi wiki hii.
  Yanga inaondoka leo, ikiwa ni siku mbili tangu iwatoe wenyeji, Ihefu FC hatua ya 32 Bora ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa ushindi wa penalti 4-3 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya juzi.
  Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, Ihefu ya Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara ilikaribia kuimaliza Yanga ndani ya dakika 90, kama si bao la penalti la dakika ya mwisho la mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa.
  Ihefu walitangulia kwa bao la kujifunga la beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ dakika ya 36 katika juhudi za kuokoa shuti la Innocent Kapalata aliyepasiwa na Elias Salingo.
  Baada ya bao hilo, Yanga waliokuwa wakicheza taratibu walikuwa kama waliopigwa mshituko na kuamka kwa kuongeza kasi ya mashambulizi.
  Lakini safu ya ulinzi ya Ihefu ikiongozwa na kipa wake hodari, Andrew Kayuni iliwazuia watoto wa kocha Mzambia, George Lwandamina kupata bao.
  Kipindi cha pili, Ihefu wakaamua kabisa kucheza kwa kujihami na huku wakipoteza muda kwa kujiangusha na kuchelewa kuanzisha mipira inapofuka upande wao.
  Lakini Yanga waliendelea kuwa wastahmilifu huku pia wakibadili mbinu moja baada ya nyingine katika jitihada za kusaka bao la kusawazisha.
  Hatimaye mpango wa kutafuta penalti wa Chirwa ukafanikiwa dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza kati ya sita baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo, pale Mzambia huyo alipoingia kwenye boksi na kwenda chini kwa urahisi baada ya kubanwa na mabeki wawili wa Ihefu.  
  Chirwa mwenyewe akaenda kufunga penalti hiyo na kuwainua kwa furaha mamia ya mashabiki wa Yanga waliokuwa wamenyong’onyea kwa pamoja na baridi ya Mbeya, lakini pia matokeo ya kuwa nyuma kwenye mchezo.
  Ukawadia muda wa matuta na kipa wa Ihefu Andrew Kayuni akawashitua Yanga baada ya kuokoa penalti ya kwanza ya Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi – lakini Nahodha Kevin Yondan akarejea kufunga ya pili, Hassan Kessy akafunga ya tatu, Gardiel Michael ya nne kabla ya Chirwa kughongesha mwanmba penalti ya tano na Raphael Daudi kufunga ya sita.
  Kipa Mcameroon, Youthe Rostand akaibuka shujaa wa Yanga baada ya kupangua penalti tatu za Abubakar Kidungwe, Emmanuel Mamba na Richard Ngondya wakati za Andrew Kayuni, Mando Mkumbwa na Jonathan Mwaibindi zilimpita na kutinga nyavuni.
  Yanga sasa inarejea kwenye Ligi Kuu baada ya kupenya kwenye ‘tundu la sindano’ kuingia 16 Bora ya ASFC ikianza na Lipuli.
  Ikumbukwe Yanga iliuanza vibaya msimu huu wa Ligi Kuu kwa kulazimishwa sare ya 1-1 na Lipuli nyumbani Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na tangu haijawa na matokeo yenye mwendelezo mzuri kiasi cha kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa inazidiwa pointi saba na mahasimu wake, Simba SC wanaoongoza.
  Yanga SC ambayo inaaminika mzunguko wa pili ndiyo hubadili gia kwenye mbio za ubingwa na kuanza kasi kubwa, imepania kuizima Lipuli Uwanja wa Samora Jumamosi.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAONDOKA LEO MBEYA KUIFUATA LIPULI LIGI KUU JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top