• HABARI MPYA

  Wednesday, February 14, 2018

  TSHISHIMBI APIGA MBILI YANGA SC YAITANDIKA MAJI MAJI 4-1 TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imejisogeza jirani na vinara, Simba SC baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Maji Maji ya Songea katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Nyota wa mchezo wa leo alikuwa kiungo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Papy Kabamba Tshishimbi aliyefunga mabao mawili, moja kila la kipindi, la kwanza na la mwisho wakati mabao mengine yalifungwa na Emmanuel Martin naq Obrey Chirwa.
  Mabingwa hao watetezi, Yanga SC sasa wanafikisha pointi 37 baada ya kucheza mechi 18, wakizidiwa pointi nne tu na wapinzani wao wa jadi, SImba wenye pointi 41, wakati Azam FC sasa ni ya tatu kwa pointi zake 34.
  Papy Kabamba Tshishimbi (kushoto) akishangilia na Emmanuel Martin (kulia) baada ya kufunga bao la mwisho la Yanga 
  Obrey Chirwa (kulia) akienda chini baada ya kuangushwa na beki wa Maji Maji, Paulo Maona
  Kiungo Ibrahim Ajib wa Yanga akipiga mpira kiufundi mbele ya beki wa Maji Maji
  Beki wa Yanga, Gardiel Michael akipasua katikati ya wachezaji wa Maji Maji
  Kiungo mtaalamu, Papy Kabamba Tshishimbi akiondoka na mpira dhidi ya beki wa Maji Maji 

  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Nassor Mwinchui wa Pwani, aliyesaidiwa na Jesse Erasmo wa Morogoro na Mashaka Mwandembwa wa Mbeya, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 3-0.
  Aliyeanzisha sherehe za mabao za Yanga leo alikuwa ni kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi aliyefunga kwa penalti dakika ya 18  baada ya Mpoki Mwakinyuke wa Maji Maji kuushuka mpira uliopigwa na Mzambia, Obrey Chirwa ambao ulikuwa unaelekea nyavuni.
  Pamoja na penalti, refa Mwinchui akamtoa nje kwa kadi nyekundu Mwakinyuke, kwani ndiye aliyekuwa mchezaji wa mwisho wakati anaokoa kwa mikono.
  Chirwa akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 29, akimalizia krosi nzuri ya beki wa kushoto, Gardiel Michael Mbaga kabla ya kuonyeshwa kadi ya njano kwa kuvua jezi kuonyesha fulana iliyoandikwa ‘Never Give Up’ wakati anashangilia bao hilo.
  Kiungo mshambuliaji, Emmanuel Martine akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 43 kwa shuti la umbakli wa mita 22.
  Kipindi cha pili, Maji Maji walikianza vizuri kwa kupeleka mashambulizi, mfululizo langoni mwa Yanga na kufanikiwa kupata lililofungwa kwa penalti na Geoffrey Mlawa dakika ya 56 baada ya beki wa Yanga, Said Juma ‘Makapu’ kuunawa mpira kwenye boksi katika harakati za kuokoa.
  Baada ya bao hilo, mchezo ulipooza kidogo na Maji Maji wakionekana kuumiliki zaidi mpira kabla ya Yanga kuzinduka dakika 10 za mwisho na kuanza kujibu mashambulizi.
  Tshishimbi aliye katika msimu wake wa kwanza Yanga tangu asajiliwe kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland, akaifungia timu hiyo bao la nne dakika ya 83 kwa shuti la umbali wa mita 20 baada ya kukutana na mpira uliorudi kufuatia kona ya winga Geoffrey Mwashiuya kuokolewa mara mbili. 
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhan Kabwili, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Said Juma ‘Makapu’, Andrew Vincent ‘Dante’, Maka Edward, Emmanuel Martin, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita/Geoffrey Mwashiuya dk71, Obrey Chirwa na Ibrahim Ajib/Juma Mahadhi dk69.
  Maji Maji FC; Saleh Malande, Aziz Sibo, Mpoki Mwakinyuke, Kennedy Kipepe, Paul Maona, Hassan Hamisi, Peter Mapunda, Yakubu Kibiga/Alex Kondo dk50, Six Mwakasega/Geoffrey Mlawa dk50, Marcel Boniventura/Lucas Kikoti dk77 na Jaffar Mohammed.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TSHISHIMBI APIGA MBILI YANGA SC YAITANDIKA MAJI MAJI 4-1 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top