• HABARI MPYA

  Monday, February 12, 2018

  SAMATTA ANAENDELEA VIZURI NA LEO AMEFANYA MAZOEZI KIKAMILIFU GENK IKIJIANDAA KUIVAA BRUGGE

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta leo amefanya mazoezi kikamilifu na klabu yake, KRC Genk kuelekea mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji dhidi ya wenyeji, Club Brugge Jumamosi  Uwanja wa Jan Breydelstadion mjini Brugge.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu leo, Samatta amesema kwamba anaendelea vizuri baada ya maumivu ya Ijumaa na leo amefanya vizuri tu na wenzake.
  “Naendelea vizuri kabisa, Ijumaa nilihisi maumivu kidogo katika mguu ule ule niliofanyiwa upasuaji, ikabidi nipumzike kuepusha maumivu zaidi. Lakini namshukuru Mungu maumivu yamepoa na nimerudi mazoezini,”amesema Samatta.
  Mbwana Samatta anaendelea vizuri Genk kuelekea mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji dhidi ya wenyeji, Club Brugge Jumamosi 

  Aidha, Samatta amesema kwamba Daktari wa timu yao amemuambia asitarajie maumivu kupoa haraka, kwani yataisha polepole – maana yake ataendeela kucheza akihisi maumivu, lakini wakati huo huo anaimarika taratibu.  
  Samatta, Nahodha wa Taifa Stars alizua hofu Ijumaa baada ya kucheza kwa dakika 36 tu kabla ya kuumia na kutolewa  Genk ikiibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Zulte-Waregem kwenye mchezo wa Ligi Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
  Siku hiyo, Samatta alitolewa dakika ya 36 na nafasi yake ikachukuliwa na mshambuliaji Mkongo, Dieumerci N'Dongala wakati huo timu hizo zikiwa zimefungana 1-1, Genk wakitangulia kwa bao la mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis dakika ya 20 kabla ya mshambuliaji Mtunisia, Hamdi Harbaoui kuisawazishia Zulte-Waregem kwa penalti dakika ya 22.
  Baada ya hapo, Genk ikafanikiwa kupata mabao mawili zaidi, yaliyofungwa na kiungo mkongwe wa umri wa miaka 36, Mbelgiji Thomas Buffel dakika ya 59 na kiungo Mspaniola, Alejandro Pozuelo Melero Pozuelo dakika ya 90 na ushei.
  Februari 9, Samatta jana alikuwa anacheza kwa mara ya tano tu tangu apone maumivu ya mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia iliyochanika Novemba 4, mwaka jana akiichezea KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren katika mchezo wa Ligi hiyo Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk na kumsababisha afanyiwe upasuaji mdogo. 
  Kwa ujumla Samatta amecheza mechi 75 tangu alipojiunga na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Na katika mechi hizo, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA ANAENDELEA VIZURI NA LEO AMEFANYA MAZOEZI KIKAMILIFU GENK IKIJIANDAA KUIVAA BRUGGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top