• HABARI MPYA

  Thursday, February 01, 2018

  NI NIGERIA NA MOROCCO FAINALI YA CHAN JUMAPILI CASABLANCA

  TIMU ya taifa ya Nigeria itakutana na wenyeji, Morocco katika fainali ya Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) Jumapili.
  Hiyo ni baada ya timu zote kushinda mechi zao za Nusu Fainal jana, Morocco wakiwatoa jirani zao, Libya na Nigeria wakiwatia Sudan saa 24 baadaye.
  Nigeria imekwenda fainali baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Sudan, bao pekee la Gabriel Okechukwu dakika ya 16 Uwanja wa Marrakech akimalizia pasi ya Anthony Okpotu kumtungua kipa Akram El Hadi.
  Super Eagles ilipata pigo katika mchezo huo mapema tu baada ya kipa wake tegemeo kwenye mashindano haya, Ikechukwu Ezenwa alipolazimika kutoka nje kufuatia kuumia baada ya kugongana na Mohamed Hashim. 
  Gabriel Okechukwu akikimbia kushangilia baada ya kuifungia Nigeria dakika ya 16 jana Uwanja wa Marrakech

  Hata hivyo, Ajiboye Oladale aliyeingia kuchukua nafasi yake akaenda kufanya kazi nzuri kwa kuokoa michomo mingi ya hatari na Super Eagles ikaenda fainali.
  Sudan nayo ilipata pigo baada ya mchezaji wake, Bakri Makki kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 87 kwa kumchezea rafu Okechukwu nje ya eneo la penalti.
  Mchezo mwingine, Libya ilijitahidi na kumaliza dakika 90 ikiwa imefungana 1-1 na Morocco Uwanja wa Mohamed V mjini Casablanca, lakini ikashindwa kumalizia dakika 30 za nyongeza kwa kujiruhusu kufungwa mabao mawili na kulala kwa 3-1 baada ya dakika 120. 
  Simba wa Atlasi walitangulia kwa bao la Ayoub El Kaabi dakika ya 73, kabla ya Abdulrhman Khalleefah kuisawazishia Libya dakika ya 86.
  Mchezo ukahamia kwenye dakika 30 za nyongeza na mabao ya Ayoub El Kaabi dakika ya 97 na Walid El Karti kwa penalti dakika ya 118 yaliwapeleka wenyeji fainali itakayofanyika Jumapili Saa 4:00 usiku Uwanja wa Mohamed V, ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu Jumamosi Saa 4:00 usiku pia Uwanja wa Marakech kati ya Sudan na Libya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI NIGERIA NA MOROCCO FAINALI YA CHAN JUMAPILI CASABLANCA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top