• HABARI MPYA

  Friday, February 02, 2018

  NDUNDA NA MBONDE KUANZA MAZOEZI WIKI IJAYO SIMBA SC

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  KIPA wa pili wa Simba, Said Mohammed 'Nduda' wiki ijayo atajiunga na wenzake tayari kuanza mazoezi baada ya kuwa nje kwa miezi mitano, kufuatia kufanyiwa upasuaji wa goti Oktoba mwaka jana nchini India.
  Na hiyo ni baada ya kipa huyo kuwa kwenye programu za mazoezi yake binafsi tangu mwanzoji mwa mwaka huu, akijifua ufukweni na gym. 
  Ikumbukwe Nduda aliyesajiliwa Simba Julai mwaka jana akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, hajacheza mechi yoyote msimu huu kutokana na maumivu ya goti aliyoyapata Agosti mwaka jana mazoezini.
  Said Mohammed 'Nduda' akijifua ufukweni kujiweka fiti kabla ya kujiunga na wachezaji wenzake wa Simba wiki ijayo 
  Said Mohammed 'Nduda' amekuwa nje kwa miezi mitano, kufuatia kufanyiwa upasuaji wa goti Oktoba mwaka jana nchini India

  Aliumia kambini visiwani Zanzibar wakati Simba inajiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wa jadi, Yanga Agosti 23, mwaka jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Simba ilivutiwa na Nduda na kumsajili baada ya kudaka vizuri katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu wa Kombe la COSAFA dhidi ya Lesotho Julai 7, mwaka jana mjini Rusternburg, Afrika Kusini Taifa Stars ikishinda kwa penalti baada ya sare ya 0-0. 
  Na Nduda akashinda tuzo ya kipa bora wa mashindano hayo baada ya kazi yake nzuri kwenye mchezo huo mmoja tu, kiasi cha kuwashawishi na Simba kumsajili na kumuunganisha na kipa namba wa Taifa Stars, Aishi Manula.
  Kipa mwingine wa Simba kwa sasa ni Emmanuel Mseja ambaye naye pia ni mpya aliyesajiliwa Julai kutoka Mbao FC ya Mwanza.
  Beki wa Simba, Salim Mbonde ameendelea na mazoezi ya gym kujiweka fiti kabla ya kuungana na wenzake

  Wakati huo huo, beki wa kati wa Simba, Salim Mbonde anaendelea na mazoezi ya gym baada ya kuwa nje kwa mwezi zaidi ya miezi mitatu kufuatia kuumia Oktoba 15, mwaka jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya timu yake ya zamani, Mtibwa Sugar uliomalizika kwa sare ya 1-1 mjini Dar es Salaam.
  Matarajio kwa Mbonde aliye katika msimu wake wa kwanza pia Simba tangu aondoke Manungu, Turiani mkoani Morogoro, maskani ya Mtibwa Sugar ni ataanza mazoezi wiki ijayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDUNDA NA MBONDE KUANZA MAZOEZI WIKI IJAYO SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top