• HABARI MPYA

  Saturday, February 17, 2018

  KAGERA SUGAR YAENDELEA KUJIKONGOJA…SARE TENA 1-1 NA SINGIDA UNITED KAITABA

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  TIMU ya Kagera Sugar imelazimishwa sare nyingine nyumbani, baada ya kufungana 1-1 na Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Matokeo hayo yanayofuatia sare nyingine ya 1-1 na Azam FC hapo hapo Kaitaba, yanaiongezea Kagera Sugar pointi moja na kufikisha 15 baada ya kucheza mechi 19, ingawa inaendelea kubaki nafasi ya 14 mbele ya Maji Maji na Njombe Mji FC zenye pointi 15 pia baada ya mechi 19.

  Wachezaji wa Kagera Sugar (kulia) wakimpongeza Mohammed Fakhi baada ya kuwafungia kwa penalti, huku Singida United wakilalamika kwa refa (kushoto)

  Katika mchezo wa leo, Kagera Sugar ya kocha Mecky Mexime ilitangulia kwa bao la beki Mohammed Fakhi kwa penalti dakika ya 33, kufuatia Michael Rusheshangoga kuunawa mpira kwenye boksi, kabla ya Kambale Salita kuisawazishia Singida United dakika ya 49.  
  Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Njombe Mji FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Maji Maji ya Songea Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe.
  Ditram Nchimbi alianza kuiadhibu timu yake ya zamani kwa kuifungia Njombe Mji FC dakika ya 50, kabla ya Aziz Sibo kuisawazishia Maji Maji dakika ya 90 na ushei. Ni matokeo hayo yanaiongezea kila timu pointi moja na kufikisha 15 sawa na Kagera Sugar iliyo juu yao kwa wastani wa mabao.  
  Ligi Kuu inatarajiwa inatarajiwa kuendelea kesho kwa mechi moja, Mbeya City wakiikaribisha Stand United Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wakati Jumatatu Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Sokoine na Mtibwa Sugar wataikaribisha Ruvu Shooting Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAGERA SUGAR YAENDELEA KUJIKONGOJA…SARE TENA 1-1 NA SINGIDA UNITED KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top