• HABARI MPYA

  Monday, February 12, 2018

  AZAM FC INA SHUGHULI NA KAGERA SUGAR UWANJA WA KAITABA LEO

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  TIMU ya Azam FC inashuka Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba leo kumenyana na wenyeji, Kagera Sugar katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Mchezo wa leo ni muhimu kwa Azam FC kusawazisha makosa yake, baada ya kupoteza mechi iliyopita wakifungwa na Simba SC 1-0 Uwanja wa Taifa. 
  Azam FC iliwasili Bukoba jana kwa ndege, tayari kabisa kuwakabili Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba
  Huu ni mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu baina ya timu hizo, baada ya Azam FC kuutumia vizurin Uwanja wa nyumbani kwenye mchezo wa kwanza kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.
  Azam FC inashuka Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba leo kumenyana na wenyeji, Kagera Sugar katika Ligi Kuu  

  Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/2014, wataendelea kuikosa huduma ya Nahodha Himid Mao ‘Ninja, aliyepewa mapumziko maalum kufuatia majeraha ya goti la mguu wa kulia yanayomsumbua, pamoja na mshambuliaji Wazir Junior na beki Daniel Amoah, ambao nao ni majeruhi.
  Aidha itamkosa nahodha wake msaidizi, Aggrey Morris, aliyekusanya kadi tatu za njano, zinazomfanya kukosa mechi moja ijayo, lakini wachezaji wengine wote waliobakia wapo fiti kwa ajili ya mchezo huo, ukiondoa majeruhi wa muda mrefu Joseph Kimwaga, ambaye anaendelea na mazoezi maalum ya kumuimarisha taratibu.
  Kwa sasa Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 33, sawa na Singida United iliyo katika nafasi ya nne, ikizidiwa pointi nane na Simba iliyojikusanyia pointi 41, mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 34 baada ya timu zote tatu kucheza mechi 17.
  Hali ni mbaya kwa Kagera Sugar, ambayo sasa inazibeba timu nyingine zote 15 katika ligi ya timu 16, ikiwa ina pointi 13 tu baada ya mechi 17.
  Mechi za jana Mbao ililazimishwa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Stand United iliichapa Singida United 1-0 Uwanja wa Namfua, Njombe Mji FC wamelazimishwa sare ya 0-0 na Mbeya City Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
  Mechi nyingine za jana, Ndanda FC imelazimishwa sare ya 0-0 na Tanzania Prisons Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara na Ruvu Shooting imeibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Lipuli Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC INA SHUGHULI NA KAGERA SUGAR UWANJA WA KAITABA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top