• HABARI MPYA

    Monday, February 20, 2017

    SERIKALI YAITAKA TFF KUTEUA MAREFA WA KUCHEZESHA HAKI SIMBA NA YANGA

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    MKURUGENZI wa Michezo, Yusuph Singo ameitaka Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutumia marefa watakaochezesha kwa haki mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga Februari 25, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mkutano maalum kuelekea mchezo wa watani wa jadi Jumamosi, Singo amewataka mashabiki kujiepusha na vurugu za aina yoyote  katika mechi hiyo kwa sababu yeyote atakayebainika kufanya kosa lolote hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. 
    “Tunatoa rai kwa waamuzi waliopewa dhamana ya kuchezesha mchezo huu, wajue kuwa wana dhamana kubwa, hivyo ni vyema wakafuata kanuni na sheria za mchezo husika ili kuepusha malalamiko,” alisema.
    Askari Polisi akiwa na mmoja wa majeruhi baada ya vurugu za Oktoba 1, mwaka jana
    Yussuph Singo (katikati) akzungumza na Waandishi wa Habari leo. Kulia ni Inspekta Hashim na Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura

    Singo amewaomba wadau wote kujenga utamaduni wa kununua tiketi mapema, kwani hadi sasa tiketi zinapatikana kupitia SELCOM na hiyo itaondoa msongamano na lawama zisizo za lazima.
    “Tunafahamu kuwa kuna changamoto za matumizi ya mfumo wa Ki- elektroniki lakini hatuna budi kuendelea kuelimishana na kujifunza kwani huko ndiko Dunia ilipo,tutakua watu wa ajabu leo tukisema hatuwezi kutumia mfumo huu kisa changamoto hizi ndogondogo zinazojitokeza,”.
    “Tujiepushe na vurugu za aina yoyote siku ya mchezo kwani Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayepelekea uvunjifu wa amani siku ya mchezo,”alisema.
    Ameongeza kwamba kutakuwa na ulinzi wa kutosha ndani na nje ya Uwanja, sambamba na kamera zenye uwezo wa kumuona kila mtu anayeingia Uwanjani na kila anachokifanya. “Tutapiga picha na kuzirusha kwenye TV kubwa ya Uwanja kwa wale wote watakaobainika kuashiria, kutenda vurugu sheria itachukua mkondo wake,”aliongeza.
    Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Boniface Wambura alisema kwamba mchezo huo utaanza saa 10.00 jioni na kwamba mwamuzi atatangazwa wakati wowote kuelekea mchezo huo.
    Alionya mashabiki kutofanya vurugu kwa sababu masharti ya kuufungulia yanakwenda sambamba na kuchunguzwa kama jamii ya wapenda soka kama imejirekebisha baada ya kutokea vurugu Oktoba mosi, mwaka jana.
    Meneja Mauzo wa Kampuni inayotoa Huduma ya Kuuza Tiketi za Elektroniki, Gallus Runyeta alisema kwamba wanatarajiwa kutoa huduma ambayo haitakuwa na changamoto kama ilivyotokea huko nyuma.
    Kwa upande wake, Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa TFF, Inspekta wa Polisi, Hashim Abdallah amesema kwamba jeshi la ulinzi na usalama litahakikisha usalama unaimarika uwanjani hapo na kwa yeyote atakayefanya fujo atachukuliwa hatua
    Ikumbukwe Serikali iliiufungia Uwanja wa Taifa kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya vurugu zilizojitokeza kwenye pambano la mahasimu hao Oktoba 1, mwaka jana na kusababisha uharibifu uliomuudhi hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
    Mashabiki wa Simba walifanya vurugu Uwanja wa Taifa Oktoba 1, mwaka huu baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu.
    Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
    Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
    Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    Oktoba 2, Wizari ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, ikasema Rais kwamba Magufuli alikuwa anautazama mchezo huo moja kwa moja kupitia Azam TV na akajionea mwenyewe vurugu na chanzo chake.
    Ikasema Rais Magufuli alikasirika mno na akataka hatua kali zichukuliwe, lakini akamtuliza na mwishowe hatua iliyochukuliwa ni kuzizuia timu hizo kutumia Uwanja huo - Serikali ilizuia pia mapato ya mchezo huo hadi ilipokata gharama za uharibifu uliosababishwa na vurugu hizo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERIKALI YAITAKA TFF KUTEUA MAREFA WA KUCHEZESHA HAKI SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top