• HABARI MPYA

    Sunday, February 19, 2017

    AZAM FC YAICHAPA 2-0 MWADUI CHAMAZI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    AZAM FC imejisogeza juu kidogo kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga usiku wa leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Ushindi huo unaifanya timu hiyo ya bilionea Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ifikishe pointi 41 baada ya kucheza mechi 23 na kuendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Simba SC wenye pointi 51 za mechi 22 na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 50 za mechi 21. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Andrew Shamba wa Pwani, aliyesaidiwa na Janeth Balama wa Iringa na Anold Bugado wa Singida, hadi mapumziko tayari Azam walikuwa mbele kwa 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dakika ya 24 kwa shuti la umbali wa mita 25 baada ya pasi ya Frank Domayo ‘Chumvi’.
    Kipindi cha pili, nyota ya Azam iliendelea kung’ara na wakafanikiwa kupata bao la pili, ambalo Mwadui walijifunga wenyewe baada ya beki wake, Iddi Mobby kujifunga.
    Kipa Shaaban Kado aliokoa vizuri shuti la mbali la Ramadhani Singano ‘Messi’ kwa kupangua lakini likamgonga Mobby aliyekuwa mbele yake na kurudi nyumbani dakika 89 kuunenepesha ushindi wa Azam.
    Mwadui walipoteza nafasi mbili dakika ya 38 shuti la winga wake, Hassan Salum Kabunda lilipodakwa na kipa Aishi Salum Manula na dakika ya 44 shuti la Miraji Athumani lilipokwenda nje ya lango la Azam.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Bruce Kangwa, Abbrey Morris, Yakubu Mohammed, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Samuel Afful dk62, Frank Domayo, Yahya Mohammed/Erato Nyoni dk88, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Joseph Mahundi/Masoud Abdallah ‘Cabaye’ dk70.
    Mwadui FC; Shaaban Kado, Nassor Masoud ‘Chollo’, David Luhende, Iddi Mobby, Malika Ndeule, Razack Khalfan, Abdallah Seseme, Awadh Juma, Paul Nonga/Salum Iyee dk18, Miraj Athuman na Hassan Kabunda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAICHAPA 2-0 MWADUI CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top