• HABARI MPYA

    Tuesday, February 28, 2017

    KOCHA AZAM ASEMA MAMBO MAZURI YANAKUJA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BAADA ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), Kocha Msaidizi, Idd Nassor Cheche, amewaambia mashabiki kuwa mambo mazuri yakuja zaidi hivyo wakae mkao wa kula.
    Azam FC imetinga hatua hiyo jana jioni baada ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0, lililofungwa na winga Ramadhan Singano dakika ya 6 akitumia vema pasi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ iliyowababatiza mabeki kabla ya mfungaji kuunasa na kupiga shuti la kiufundi lililompita kipa wa Mtibwa, Saidi Mohammed.
    Cheche alisema jana mjini Dar es Salaam kwamba haikuwa kazi rahisi wao kutinga hatua hiyo kutokana na kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Mtibwa Sugar, lakini hali ya kupambana ya wachezaji wake muda wote wa mchezo iliweza kufanikisha hilo.
    “Kwanza tunammshukuru Mungu kwa kupata ushindi huu, mchezo haukuwa rahisi tumepambana hadi mwisho hadi kupata matokeo, napenda kuwaambia mashabiki na wapenzi wote wa Azam FC kuwa mambo mazuri yanakuja, kazi si rahisi lakini tunajitahidi kupambana ili tuhakikishe timu yetu inafika katika hali ya juu kabisa,” alisema.
    Alisema kadiri wanavyosonga mbele, michuano  hiyo inazidi kuwa migumu na kudai kuwa watazichukulia kwa uzito mechi zote watakazocheza ili kutwaa ubingwa na kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
    “Michuano hii inavyokuwa migumu na wewe kadiri unavyocheza mechi, hiyo inazidi kukupa uzoefu kuelekea raundi inayofuata, kwa sababu unapocheza unakuwa unafanya makosa na unapoyafanyia kazi ndio unavyozidi kujiweka vizuri zaidi, kwa hiyo hilo suala tunalifanyia kazi na tuko makini nalo, kwa sababu tunaamini haya mashindano ndio pekee tuliyobakiwa nayo ya kugombea nafasi ya kuiwakilisha nchi,” alisema.
    Msimu uliopita Azam FC ilifika fainali, lakini iliteleza baada ya kufungwa mabao 3-0 na Yanga na katika hatua hii ya 16 bora iliwatoa Panone ya Kilimanjaro 2-1, mchezo uliofanyika Uwanja wa Ushirika mkoani humo.
    Mara baada ya mtanange huo, kikosi cha Azam FC kitaanza tena mazoezi Jumatatu ijayo kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Stand United utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA AZAM ASEMA MAMBO MAZURI YANAKUJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top