• HABARI MPYA

    Tuesday, February 21, 2017

    KIKAO CHA KUTEUA MAREFA WA SIMBA NA YANGA KUFANYIKA ALHAMSI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Waaamuzi inatarajiwa kukutana keshokutwa Alhamisi mjini Dar es Salaam kuteua marefa wa kuchezesha mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga.
    Miamba hiyo ya soka ya nchini inatarajiwa kumenyana Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    Na Ofisa wa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas Mapunda ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Kamati ya Waamuzi itakutana Alhamisi kuteua marefa.
    Mapunda amesema kwamba Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Salum Chama anatarajiwa kuwasili kesho kutoka Bukoba mkoani Kagera kwa ajili ya kuongoza kikao hicho.
    Amesema Chama ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Soka Kagera (KRFA) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ataongoza kikao cha kupitia majina ili kuteua marefa wa mchezo huo.
    “Baada ya kikao chao, Kamati ya Waamuzi itawasilisha majina TFF ambayo itayapitia na kuidhinisha au kutoa maelekezo mengine, lakini nina uhakika hadi kufika Ijumaa marefa watakuwa wametajwa,”alisema Lucas.
    Zote Simba na Yanga kwa sasa zipo kambini kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi, unaofuatia ule wa Oktoba 1, mwaka huu ambao zilitoka sare ya 1-1.
    Yanga ambayo bao lake lilifungwa na Amissi Tambwe Oktoba 1, imeweka kambi Kigamboni, Dar es Salaam, wakati Simba iliyosawazisha kupitia kwa Shiza Kichuya imeweka kambi visiwani Zanzibar.
    TFF imekuwa makini katika uteuzi wa marefa wa mchezo wa Jumamosi, baada ya vurugu zilizojitokeza kwenye pambano la Oktoba 1, mwaka jana na kusababisha uharibifu uliomuudhi hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kiasi cha kuzizuia timu hizo kutumia Uwanja huo kwa miezi mitatu.
    Mashabiki wa Simba walifanya vurugu Uwanja wa Taifa Oktoba 1, mwaka huu baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu.
    Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
    Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
    Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    Oktoba 2, Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, ikasema kwamba Rais Magufuli alikuwa anautazama mchezo huo moja kwa moja kupitia Azam TV na akajionea mwenyewe vurugu na chanzo chake na alikasirika mno na kuagiza hatua kali zichukuliwe.
    Wizara ikazizuia timu hizo kutumia Uwanja huo pamoja na kuzuia mapato ya mchezo huo hadi ilipokata gharama za uharibifu uliosababishwa na vurugu hizo. Mwishoni mwa mwezi uliopita Serikali ikaziruhusu timu hizo kutumia tena Uwanja huo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIKAO CHA KUTEUA MAREFA WA SIMBA NA YANGA KUFANYIKA ALHAMSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top