• HABARI MPYA

    Saturday, February 25, 2017

    MWISHO WA UBISHI SIMBA NA YANGA TAIFA LEO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    HATIMAYE baada ya majigambo na kujipiga kifua, leo miamba ya soka Tanzania, Simba na Yanga inamaliza ubishi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Mchezo huo uliopewa uangalizi wa ziada na Serikali na Jeshi la Polisi, unafuatia ule wa mzunguko wa kwanza uliomalizika kwa sare ya 1-1 Oktoba 1, mwaka jana, Yanga wakitangulia kwa bao la Amissi Tambwe dakika ya 26, kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba dakika ya 86.
    Lakini tu mchezo wa Oktoba 1 uliingia doa baada ya vurugu za mashabiki wa Simba, vurugu zilizojitokeza na kusababisha uharibifu uliomuudhi hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na kusababisha Serikali kuufungia Uwanja wa Taifa kwa zaidi ya miezi mitatu.
    Refa Martin Saanya nyuma ya viungo, Muzamil Yassin wa Simba (kulia) na Juma Mahadhi wa Yanga (kushoto)

    Mashabiki wa Simba walifanya vurugu Uwanja wa Taifa Oktoba 1, mwaka jana baada ya Tambwe kuifungia bao la kuongoza Yanga, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    Oktoba 2, Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, ikasema Rais kwamba Magufuli alikuwa anautazama mchezo huo moja kwa moja kupitia Azam TV na akajionea mwenyewe vurugu na chanzo chake.
    Ikasema Rais Magufuli alikasirika mno na akataka hatua kali zichukuliwe, lakini akamtuliza na mwishowe hatua iliyochukuliwa ni kuzizuia timu hizo kutumia Uwanja huo - Serikali ilizuia mapato ya mchezo huo hadi ilipokata gharama za uharibifu uliosababishwa na vurugu hizo.
    Uwanja wa Taifa sasa umefungwa kamera maalum za kumuona kila anayeingia na anachokifanya na leo kutakuwa na ulinzi mkali. Lakini pia, Serikali na Polisi wameomba marefa walioteuliwa kuchezesha mechi hiyo, Methew Akrama wa Mwanza, atakayesaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga na Hassan Zani wa Arusha watakaopeperusha vibendera pembezoni mwa Uwanja kutenda haki.
    Yanga itaingia kwenye mchezo wa leo ikitokea Kimbiji Kigamboni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wakati Simba inatokea Zanzibar na iliwasili jana Dar es Salaam.
    Mchezo wa leo utakuwa wa 40 kwa kocha Mcameroon, Joseph Omog Simba SC, kati ya hiyo 22 ni ya Ligi Kuu nyingine za kirafiki na vikombe mbalimbali, akiwa ameshinda mechi 28 moja kwa penalti baada ya sare ya 0-0 na Yanga Kombe la Mapinduzi Januari 10, mwaka huu. 
    Omog amefungwa mechi sita tangu atue Simba Julai mwaka jana, mbili kati ya hizo akifungwa na timu yake ya zamani, Azam moja katika Kombe la Mapinduzi na nyingine Ligi Kuu, wakati tano ametoa sare.
    Kwa Mzambia wa Yanga, aliyewasili Novemba mwaka jana, amefungwa mechi tatu kati ya 14 alizocheza, kipigo kikubwa zaidi kikitoka kwa Azam 4-0 Kombe la Mapinduzi. Ameshinda mechi tisa ikiwemo moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika 5-1 dhidi ya Ngaya Club de Mde ya Comoro na mbili ametoa sare, zote 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya African Lyon na Ngaya Clube de Mde.  
    Mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi (matano) kwenye mechi za watani kati ya wachezaji wa sasa akiwa anajivunia kucheza timu zote, Simba na Yanga. Tambwe amefunga mabao matano, mawili akiwa Simba na matatu akiwa Yanga. 
    Akiwa Simba alifunga katika mechi ya Nani Mtani Jembe Desemba 23, mwaka 2013 mabao mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Yanga dakika za 14 na 44 kwa penalti, lingine likifungwa na na Awadh Juma, wakati la Yanga lilifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 87.  
    Akiwa Yanga alifunga bao la kwanza Septemba 26, mwaka 2015 katika ushindi wa 2-0 dakika ya 44, kabla ya Malimi Busungu kufunga la pili dakika ya 79, akafunga tena la pili dakika ya 72 katika ushindi wa 2-0 Februari 20, mwaka 2016 baada ya Donald Ngoma kufunga la kwanza dakika ya 39 na Oktoba 1, 2016 akafunga la kwanza dakika ya 26 katika sare ya 1-1, kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba dakika ya 87.
    Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ndiye mchezaji wa muda mrefu zaidi Yanga na kwa ujumla kwenye mechi za watani wa jadi. Alijiunga na Yanga mwaka 2006, akitokea Malindi ya kwao, Zanzibar kabla ya mwaka 2009 kwenda kwa mkopo wa nusu msimu Vancouver Whitecaps ya Canada na kurejea Jangwani, anakoendelea na kazi hadi sasa. 
    Hata hivyo, Cannavaro hana uhakika wa namba kwa sasa kwenye kikosi cha Yanga, kutokana na ujio wa beki wa Andrew Vincent msimu huu, anayefanya idadi ya mabeki watano wa kati katika timu hiyo, wengine wakiwa ni Kevin Yondan, Pato Ngonyani na Vincent Bossou kutoka Togo. 
    6-0 unabaki kuwa ushindi mkubwa zaidi kwenye mechi za watani, ambazo Simba waliifunga Yanga Julai 19, mwaka 1977 Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru, Dar es Salaam, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ akiweka rekodi ambayo haijavunjwa ya kufunga hat trick dakika za 10, 42 na 89, mabao mengine yakifungwa na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73 huku Suleiman Said Sanga akijifunga dakika ya 20 kuipa Simba bao lingine kufanya 6-0. 
    Zaidi ya hapo, Yanga iliifunga 5-0 Simba Juni 1, mwaka 1968 mabao ya Maulid Dilunga dakika ya 18 kwa penalti na 43, Salehe Zimbwe dakika za 54 na 89 na Kitwana Manara dakika ya. 86 na Simba ikaifunga Yanga 5-0 Mei 6, mwaka 2012 mabao ya Emmanuel Okwi dakika yaa pili na 62, Felix Sunzu kwa penalti dakika ya 56, Juma Kaseja kwa penalti dakika ya 67 na Patrick Mafisango kwa penalti dakika ya 72.
    Mchezaji mmoja tu muhimu atakosekana Yanga leo, ambaye ni mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma anayesumbuliwa na maumivu ya goti, lakini wengine wote wapo fiti. Upande wa Simba, beki Mzimbabwe pia, Method Mwanjali aliyekuwa anatiliwa shaka kutokana na maumivu ya kifundo cha mguu, yuko fiti kucheza.
    Vikosi vya leo vinaweza kuwa; Simba SC; Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammwd Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Muzamil Yassin, James Kotei, Laudit Mavugo, Juma Luizio na Ibrahim Hajib.  
    Katika benchi wanaweza kuwapo Peter Manyika, Hamad Juma, Novatus Lufunga, Juuko Murshid, Said Ndemla, Mohammed Ibrahim, Shiza Kichuya, Moses Kitundu, Mwinyi Kazimoto na Pastory Athanas.
    Yanga SC; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Justin Zulu, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe na Deus Kaseke.
    Katika benchi wanaweza kuwapo; Benno Kakolanya, Hassan Kessy, Oscar Joshua, Andrew Vincent, Haruna Niyonzima, Said Juma ‘Makapu’, Geoffrey Mwashiuya, Yussuf Mhilu, Emmanuel Martin, Malimi Busungu na Matheo Anthony.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWISHO WA UBISHI SIMBA NA YANGA TAIFA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top