• HABARI MPYA

    Sunday, February 26, 2017

    PENALTI, KADI NYEKUNDU NA BADO WAMEPIGWA, WATAMLAUMU REFA HAPO?

    SIMBA jana wamefanikiwa kuwafunga kwa mara ya pili mfululizo watani wao wa jadi, Yanga baada ya kuwachapa 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    Shujaa wa Simba jana alikuwa winga Shiza Ramadhani Kichuya, aliyefunga bao la ushindi dakika za lala salama, akitoka kupika la kusawazisha.
    Ushindi huo unaifanya Simba ifikishe pointi 54 baada ya kucheza 23, ikiendelea kuongoza Ligi mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 49 za mechi 22.
    Na huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Simba dhidi ya Yanga, baada ya Januari 10 kushinda pia kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, visiwani Zanzibar.
    Kichuya aliyempokea beki Novatus Lufunga dakika ya 55, kwanza alimsetia mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo kuifungia bao la kusawazisha Simba dakika ya 66 kabla ya yeye mwenyewe kufunga la ushindi dakika ya 81.
    Ikumbukwe Kichuya ndiye aliyeifungia Simba bao la kusawazisha dakika ya 86 Oktoba 1, mwaka jana timu hizo zikitoka sare ya 1-1 baada ya Amissi Tambwe kutangulia kuifungia Yanga dakika ya 26 kwa makosa ya Lufunga tena.
    Na jana Yanga SC walitangulia kwa bao la mapema tu dakika ya tano la Simon Msuva kwa mkwaju wa penalti, baada ya kiungo Mzambia, Obrey Chirwa kuangushwa kwenye boksi na Lufunga. 
    Refa asiyejiuliza mara mbili katika maamuzi yake, Methew Akrama wa Mwanza alimtoa nje kwa kadi nyekundu beki Mkongo wa Simba, Janvier Besala Bokungu dakika ya 55 baada ya kumuonyesha kadi ya pili ya njano kufuatia kumchezea rafu Chirwa.
    Akrama alikuwa mwiba kwa timu zote mbili jana kutokana na maamuzi yake ya kufuata sheria 17 za soka bila kusita pale tu lilipotokea kosa, hali ambayo ilisababisha wachezaji wenyewe waamue kuwa na nidhamu uwanjani.
    Yanga ndiyo waliuanza vizuri mchezo huo wakitawala sehemu ya kiungo, iliyokuwa ikiundwa na wageni watupu, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mzimbabwe Thabani Kamusoko na Mzambia Justin Zulu.
    Na Simba iliyoanza na washambuliaji watatu, Mavugo, Juma Luizio na Ibrahim Hajib ikajikuta imeelemewa mno katika dakika 30 za mwanzo za mchezo.
    Yanga watajilaumu wenyewe kwa kucheza mchezo wa ‘kibishoo’ zaidi, wakigongeana pasi zisizo na tija badala ya kusaka mabao moja kwa moja.  
    Kibao kilianza kuigeukia Yanga baada ya kocha Joseph Omog kumpunguza mshambuliaji mmoja, Luizio na kumuingiza kiungo Said Hamisi Ndemla dakika ya 27 aliyekwenda kuipa uhai timu yake.
    Na Yanga ikapata pigo baada ya kiungo wake tegemeo, Kamusoko kuumia na kumpisha Said Juma ‘Makapu’ dakika ya 45.
    Kipindi cha pili, Simba SC ilirudi na maarifa mapya na pamoja na mabadiliko mengine yaliyofanywa na Omog, akiwatoa Lufunga na Mohammed Ibrahim na kuwaingiza Mkude na Kichuya mambo yakawa mazuri upande wao.
    Pamoja na kumpoteza Bokungu aliyetolewa kwa kadi nyekundu, lakini Simba wakatoka nyuma na kushinda 2-1.
    Kichuya alimtilia krosi maridadi Mavugo kutoka kulia akafunga kwa kichwa dakika ya 66 kabla ya yeye mwenyewe kupiga shuti kutoka umbali wa mita 20 kuifungia bao la ushindi Simba dakika ya 81.
    Kilichoonekana katika mchezo wa jana ni matunda ya maandalizi mazuri kwa Simba kuanzia nje hadi ndani ya Uwanja na dhamira halisi ya ushindi.
    Na sifa zaidi zimuendee kocha Omog kwa maamuzi yake ya haraka ya kubadilisha mfumo kutoka kutumia washambuliaji watatu hadi wawili ili kuongeza idadi ya viungo kutoka watatu hadi wanne.
    Lakini hata upangaji wake wa timu, ulikuwa na mtiririko mzuri – kwa kuujua ugumu wa mechi aliacha wachezaji wa kuingia kubadilisha mchezo baadaye na hilo lilifanikiwa.
    Tangu yupo Azam, Omog ni kocha ambaye huwa anajua mwenyewe anachokifanya na japokuwa si mara zote hupatia, lakini mara nyingi hesabu zake hulipa – kama jana.
    Mrundi Amissi Tambwe alilazimishwa kucheza akiwa anaumwa goti na Mzimbabwe Donald Ngoma alikosekana Yanga kwa sababu ya majeruhi na pale nyuma beki Mtogo Vincent Bossou akakosekana pia. Yanga ilipungukiwa watu muhimu.
    Simba ilimkosa beki wake tegemeo wa kati, Method Mwanjali raia wa Zimbabawe aliyekuwa majeruhi pia. Ilimkosa mtu muhimu.
    Na usajili waliofanya kuanzia Julai Yanga wanaujua wenyewe, wamesajili wachezaji wengi ambao hawana tija kwa timu – basi kipigo ilikuwa halali yao jana.
    Yanga ilikufa baada ya kuumia Kamusoko, ambaye ndiye alikuwa akiichezesha timu vizuri sana. Niyonzima kama kawaida yake, mechi za Simba huwa zinamsumbua. Mara chache sana Haruna akafanya vizuri dhidi ya Simba.
    Wachezaji wa Yanga walikuwa wanafanya makosa mengi jana yenye kuwapa nafasi za kufunga Simba, japokuwa mwelekeo wa mchezo ulikuwa vizuri kwao.
    Walipata bao la mapema la penalti, wakapunguziwa nguvu ya wapinzani kwa Bokungu kutolewa kwa kadi nyekundu, lakini bado wamepigwa. Watamlaumu refa hapo? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PENALTI, KADI NYEKUNDU NA BADO WAMEPIGWA, WATAMLAUMU REFA HAPO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top