• HABARI MPYA

    Friday, June 10, 2016

    YANGA WAENDA KAMBINI UTURUKI JUMAPILI, KESSY NA WAPYA WOTE WANAKWENDA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA inaondoka Jumapili kwenda Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia Juni 19, mwaka huu.
    Mchezo huo wa Kundi A utafanyika Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria na Yanga itawasili nchini humo siku mbili kabla ya mechi.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kwamba wachezaji wote wakiwemo wapya waliosajiliwa hivi karibuni watasafiri.
    Wapya ni kipa Benno Kakolanya kutoka Prisons ya Mbeya, mabeki Hassan Kessy kutoka Simba, Andrew Vincent ‘Dante’ kutoka Mtibwa Sugar na kiungo Juma Mahadhi kutoka Coastal Union.
    Viungo wa Yanga Said Juma 'Makapu' (kulia) na Juma Mahadhi (kushoto) wakiwania mpira mazoezini leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam 

    Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
    Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.
    Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.
    Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.
    Kikosi kamili cha Yanga kinachokwenda Uturuki ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’, Benedicto Tinocco na Benno Kakolanya.
    Mabeki; Juma Abdul, Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
    Viungo; Thabani Kamusoko, Salum Telela, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
    Washambuliaji; Donald Ngoma, Malimi Busungu, Matheo Anthony, Amissi Tambwe na Paul Nonga.
    Msafara utaongozwa na Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja; Hafidh Saleh.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAENDA KAMBINI UTURUKI JUMAPILI, KESSY NA WAPYA WOTE WANAKWENDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top