• HABARI MPYA

    Thursday, June 23, 2016

    SIMBA SC YAWACHUKUA KOCHA NA MENEJA WA ZAMANI AZAM FC

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM 
    KLABU ya Simba inatarajiwa kumtangaza Meneja wa zamani wa Azam FC, Patrick Kahemele kuwa Mtendaji wake Mkuu.
    Aidha, Simba inatarajiwa kumtangaza kocha wa zamani wa Azam FC, Mcameroon, Joseph Marius Omog kuwa kocha mpya Mkuu wa klabu hiyo.
    Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Simba kinatarajiwa kupokea pendekezo la kuajiriwa kwa Kahemele kuwa Mtendaji Mkuu wa klabu usiku huu pamoja na Omog kuwa kocha Mkuu.
    Na kutokana na Kahemele kuungwa mkono na Wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji, baada ya kazi nzuri aliyowahi kuifanya akiwa Azam FC – kuna matarajio makubwa dili hilo litafanikiwa.
    Patrick Kahemele (kushoto) akiwa na Rais wa Simba Sc, Evans Aveva (kulia)
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE usiku huu, Kahemele amesema kwamba amefanya mazungumzo na uongozi wa Simba na kufikia makubaliano, lakini bado hajapewa Mkataba.
    “Ni kweli, nimefanya mazungumzo na uongozi wa Simba, na kimsingi tumefikia makubaliano ila bado hatujaingia Mkataba,”amesema.
    Pamoja na hayo, habari zaidi zinasema Kahemele amewasaidia Simba SC kumpata kocha wa zamani wa Azam FC, Mcameroon Joseph Marius Omog.
    Joseph Marius Omog anakuja Simba SC

    “Kahemele ni kiongozi wa kisasa kabisa, mweledi, mchapakazi na mbunifu. Tunaamini atarudisha heshima ya Simba. Hapa hajaanza kazi, lakini ametusaidia vizuri katika mchakato wa kupata kocha,”kimesema chanzo kutoka Simba.
    Simba imekuwa haina kocha Mkuu tangu Januari mwaka huu alipoondoka Muingereza, Dylan Kerr mara baada ya kuajiriwa Kocha Msaidizi, Mganda Jackson Mayanja ambaye sasa atafanya kazi chini ya Omog.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAWACHUKUA KOCHA NA MENEJA WA ZAMANI AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top