• HABARI MPYA

    Thursday, June 30, 2016

    OMOG AWASILI LEO KUSAINI MKATABA SIMBA SC

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mcameroon, Joseph Marius Omog anatarajiwa kuwasili usiku wa leo kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho na uongozi wa Simba kabla ya kusaini Mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha klabu hiyo.
    Omog na Simba SC wamefikia makubaliano baada ya mazungumzo ya awali kwa njia ya simu na barua pepe na Mcameroon huyo amekubali kuja kusaini Mkataba Dar es Salaam baada ya kutumiwa tiketi.
    Simba itakuwa klabu ya pili kwa Omog kufundisha Tanzania baada ya awali kuwa na Azam FC, aliyoiongoza kwa msimu mmoja na nusu ikishinda mechi 30 kati ya 55 za mashindano yote, sare 14 na kufungwa 11.
    Kocha Omog anakuja usiku wa leo kuanza kusaini Mkataba Simba SC
    Mwalimu huyo aliyeipa Leopard FC ya Kongo Brazaville Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2014, enzi zake alichezea Yaounde na ni mwalimu wa kiwango cha juu cha ufundishaji soka na mazoezi ya viungo aliyehitimu vizuri mafunzo yake katika Chuo cha Vijana na Michezo, INJS mjini Yaounde, Cameroon. 
    Alikwenda kujiendeleza kielimu nchini Ujerumani na kwa pamoja na Pierre Njili na Martin Ndtoungou walipata Stashahada za ukocha na leseni za UEFA daraja la B mwaka 1987. 
    Aliporejea nchini mwake, Joseph Marius Omog, alifundisha timu kadhaa kama Fovu ya Baham na Aigle ya Menoua na akazifikisha fainali ya Kombe la Cameroon klabu zote. 
    Mwaka 2001 aliteuliwa kuwa Msaidizi wa kocha Mjerumani, Winfried Schafer katika timu ya taifa ya Cameroon, Simba Wasiofungika chini ya Nahodha Samuel Eto’o haswa kutokana na kujua kwake Kijerumani, kwa sababu kocha huyo alikuwa hazungumzi Kiingereza wala Kifaransa, lugha zinazotumika nchini humo. 
    Mwaka 2003 aliteuliwa kuwa kocha Mkuu wa timu ya taifa baada kuondoka kwa Winfried Schafer, lakini akafukuzwa mwaka 2010 kutokana na matokeo mabaya na kushindwa kuiwezesha Cameroon kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
    Akaamua kutoka nje ya nchi na mwaka 2011 alijiunga na AC Leopard ya Kongo, ambayo aliiwezesha kutwaa Kombe mwaka huo huo na kuipa tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho. 
    Na akafanikiwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe hilo la Afrika mwaka 2012 kwa kuifunga Djoliba ya Mali mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano na kutengeneza ushindi wa jumla wa 4-3. Mwaka 2014 alijiunga na Azam FC ambayo aliipa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu.  
    Je, mafanikio hayo atayahamishia Simba? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OMOG AWASILI LEO KUSAINI MKATABA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top