• HABARI MPYA

    Friday, June 24, 2016

    TFF YASEMA YANGA ILIKAIDI KUTUMA WAWAKILISHI SEMINA YA MWONGOZO CAF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kwamba Yanga SC ilikataa kutuma wawakilishi kwenye warsha maalum ya Shirikisho la Soka Africa (CAF) kwa ajili ya ushiriki wao katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
    Katika taarifa yao kwa vyombo vya Habari leo, TFF wametoa ufafanuzi juu ya taarifa za upotoshaji kuhusu uratibu na ushiriki wa Yanga katika Kombe la Shirikisho.
    TFF imesema imekuwa likitoa kila aina ya mwongozo na elimu kuisaidia Yanga na hata Azam kabla haijatolewa kwenye Kombe la Shirikisho hatua za awali mwaka huu. 
    Ikumbukwe, Yanga walianzia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambako walipotolewa hatua ya 16 Bora wakaingia kwenye kapu la kuwania kucheza ya makundi ya Kombe la Shirikisho, ambako walifuzu.
    Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji (kushoto) na Makamu wake, Clement Sanga (kulia)
    TFF imesema Aprili 21, mwaka huu CAF lilituma waraka kwa timu zilizokuwa zinawania kuingia hatua ya makundi ya michuano yake (Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho) kupeleka majina ya maofisa watakaohudhuria warsha ya namna ya kuratibu mechi hizo kuelekea fainali sambamba na vivuli vya hati zao za kusafiria.
    "Maofisa walihitajika ni meneja wa timu, daktari wa timu na ofisa habari wa timu. Taarifa hiyo ilikuja kabla ya Yanga hawajacheza na Esperanca ya Angola na tukwataarifu Yanga mapema kwa kuwataka watuma nyaraka hizo kati ya Aprili 26 na Aprili 28, mwaka huu,"imesema taarifa ya TFF.
    "Lengo la warsha ilikuwa ni kujadili masuala ya uratibu, ufundi, udhamini na kanuni za mashindano. CAF ilijitolea kugharamia usafiri, malazi na gharama zote kwa watu watatu kutoka Yanga,".
    "Taarifa hizi na hata ukumbusho (reminders) zilipelekwa kwa baruapepe, simu na hata kuonana ana kwa ana kwa Katibu Mkuu wa Yanga, Ofisa Habari na Viongozi wengine wa klabu,".
    "Maofisa wa TFF kwa nyakati tofauti tofauti waliwasihi Yanga na pia kuwakumbusha kutuma majina CAF na vivuli vya hati hati ya kusafiria, lakini kwa sababu wanazoweza kuzielezea wenyewe kwa nini hawakupeleka majina."
    "Mei 22, 2016 ikiwa ni siku mbili kabla ya warsha kuanza hapo Mei 24, 2016, Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans, Bwana Baraka Deusdedit alituma majina CAF yakiwa hayana vivuli yaani photocopies vya hati ya kusafiria,".
    "Siku moja kabla ya washiriki kuanza kuwasili Cairo, Misri, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga alituma nyaraka kama zilivyotakiwa na wakatumiwa tiketi tatu (3) na CAF. Pamoja na tiketi kuletwa Yanga bado watu hao hawakusafiri wakidai klabu haijatoa ruhusa,".
    Maofisa wa TFF wamekuwa wakifanya kazi mpaka muda wa ziada wakiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ili timu iweze kushiriki vema pamoja na upungufu wa kiutawala ndani ya sekretarieti yake yanayojidhihirisha wazi," imesema taarifa ya TFF.
    TFF imeongeza kwamba masuala yote yanayolalamikiwa na Mkuu wa Idara ya Habari ya Yanga SC, Jerry Muro yaliyotolewa kwa timu zote kwenye semina ya Cairo, Misri na kwamba TFF itaendelea kuzisaidia klabu kujenga weledi kupitia mradi wa leseni za klabu na vilevile kuratibu ushiriki wa mashindano mbalimbali.
    Pamoja na hayo, TFF imeonya; "Hata hivyo, TFF haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa maofisa wa klabu wanaochafua jina la shirikisho ili kuficha madhaifu yao ya kiutawala,"imesema taarifa hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YASEMA YANGA ILIKAIDI KUTUMA WAWAKILISHI SEMINA YA MWONGOZO CAF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top