• HABARI MPYA

  Friday, June 10, 2016

  ATUEPELE: NIKO TAYARI KUSAINI SIMBA, NA MKOME KUNIZUSHIA UYANGA, HAPA KAZI TU

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MFUNGAJI bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Kombe la Azam Sports Federation (ASFC), Atupele Green Jackson amesema kwamba yuko tayari kusaini Simba wakimfuata.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Atupele amesema kwamba anashangazwa na uvumi kwamba yeye hawezi kuchezea Simba kwa madai eti ana mapenzi na Yanga.
  “Ninashangazwa sana na huu umbeya. Mimi ni mchezaji na soka ndiyo ajira yangu, niko tayari kusaini timu yoyote, nachoangalia ni maslahi,”amesema.
  Atupele Green (kushoto) akikabidhiwa tuzo ya ufungaji bopra Kombe la ASFC na Ofisa wa TFF, Jemedari Said (kulia). Katikati ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Wilfred Kidao

  Hata hivyo, Atupele amesema hajawahi kuwa na mapenzi na timu yoyote nchini zaidi ya kuipenda soka tu.
  “Mimi Yanga nilipita nikiwa mdogo na sikukaa sana, nilipoona umri wangu sasa umefikia kucheza Ligi na pale siwezi kupata nafasi, nikaenda timu nyingine nimecheza nimekuza uwezo wangu na kupata uzoefu wa kutosha na sasa watu wanamjua Atuepel ni nani,”.
  “Sisi wachezaji tunapotafuta sehemu ya kutokea, tunaweza kwenda timu yoyote ambayo tunaona tunaweza kupata nafasi ili tuinuke na wala si kwa sababu ya mapenzi,” ameongeza.
  Atupele amesema Simba kama wanamtaka wamfuate kwa mazungumzo na kama wakiafikiana basi watamhukumu kwa shughuli yake uwanjani.
  “Mimi kama mchezaji kazi yangu inaonekana uwanjani, waje tuzungumze, tukikubaliana tuingie Mkataba halafu waone kazi yangu siku tukikutana na hao Yanga,”amesema mchezaji huyo aliyemaliza Mkataba wake Ndanda FC ya Mtwara.
  Atupele aliyewahi kuchezea Yanga B baada ya kusajiliwa kwa dau la rekodi kwa wachezaji vijana, Sh. Milioni 17, amecheza Ndanda FC kwa msimu mmoja tu akitokea Kagera Sugar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ATUEPELE: NIKO TAYARI KUSAINI SIMBA, NA MKOME KUNIZUSHIA UYANGA, HAPA KAZI TU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top