• HABARI MPYA

    Saturday, June 25, 2016

    YANGA WAREJEA KWA MAFUNGU, KUNDI LA KWANZA TAYARI LIPO DAR, LINGINE…

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSAFARA wa kwanza wa Yanga umerejea Dar es Salaam Alfajiri ya leo kutoka Antalya, Uturuki, walipokuwa wameweka kambi kujiandaa na mchezo dhidi ya TP Mazembe ya DRC Jumanne.
    Yanga watakuwa wenyeji wa mabingwa wa mara tano Afrika, TP Mazembe Jumanne kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa pili wa Kundi A, Kombe la Shirikisho Afrika.
    Na msafara wa kwanza umewasili Alfajiri, wakati kundi lingine litawasili usiku wa leo na kesho kikosi kizima kitakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mazoezi.
    Baadhi ya nyota wa Yanga waliokuwa kambini Uturuki, kutoka kulia ni Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Deus Kaseke
    Huo utakuwa mchezo wa pili wa Kundi A kwa Yanga, baada ya Jumapili kufungwa 1-0 na wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia Jumapili.
    Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa watatu kutoka nchi tatu tofauti kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
    Hao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.
    Ukuta; Kutoka kulia kipa Deo Munishi 'Dida' na mabeki Vincent Bossou na Kevin Yondan 
    Kikosi kamili cha Yanga kilichokuwa kambini mjini ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.
    Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
    Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Godfrey Mwashiuya na Obrey Chirwa.
    Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.
    Msafara upo chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAREJEA KWA MAFUNGU, KUNDI LA KWANZA TAYARI LIPO DAR, LINGINE… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top