• HABARI MPYA

  Wednesday, June 15, 2016

  UGONJWA WA SIMBA UNAPOANZA KUIINGIA YANGA TARATIBU!

  HADI mwaka 2011, Simba ilikuwa timu bora zaidi nchini ikiwa na mseto mzuri wa wachezaji chipukizi, wa umri wa kati na wakongwe.
  Na vizuri zaidi ikawa na timu bora ya vijana waliyoitumia kupata nyota wengine wa kikosi cha baadaye.
  Lakini ukaingia ulevi wa ajabu, viongozi wakaanza kugombana na wachezaji na kuwafukuza kwa kesi zenye kutatulika kwa njia nyepesi tu, kama kuwakata mishahara na kadhalika.
  Walifukuzwa akina Felix Sunzu, Amir Maftah, Haruna Moshi, Juma Nyosso na wengine wakati Mussa Mgosi akiwa katika kiwango kizuri akauzwa bila kupenda DC Motema Pembe, tena kwa bei ndogo tu.

  Wakati huo huo wachezaji Mbwana Samatta na Patrick Ochan wakanunuliwa na TP Mazembe na Shomary Kapombe akaenda Ufaransa kabla ya kuibukia Azam FC.
  Watu wanakumbuka, kabla ya kifo chake, Patrick Mafisango tayari kulikuwa kuna tetesi za angeachwa kwa utovu wa nidhamu.
  Na aliwahi kukaribia kuachwa kwenye safari ya mechi ya michuano ya Afrika kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, bahati nzuri yakaisha akaenda na aliporudi ndipo akakautwa na umauti.
  Ugonjwa wa kufukuza ukahamia hadi kwa wachezaji vijana wadogo kama Haroun Chanongo na tabia ikaendelea wakawa wanafukuzwa wachezaji wengi Simba kila msimu.
  Huwezi kujua haswa sababu za kuachwa kwa wachezaji kama Amri Kiemba, Elias Maguri, Amissi Tambwe, Abdallah Seseme, Edward Christopher, Miraj Adam na wengine.
  Ilikuwa kama Simba walilewa mafanikio na baada ya hali hiyo ya fukuza fukuza wachezaji wengine wakaanza kuhofia kama Kevin Yondan na Ramadhani Singano ‘Messi’ wakaondoka wakiogopa yasije kuwakuta na wao ya kutupiwa mizigo nje.
  Sasa Simba inasota kupata timu imara ile iliyokuwa tishio hadi mwaka 2011. Simba ilikuwa ina hadi timu imara ya vijana, iliyofunga vikosi vya kwanza vya timu za Ligi Kuu za Azam FC na Mtibwa Sugar na kutwaa Kombe la Banc ABC, leo vipi pale Msimbazi?
  Wakati Simba wanajutia ‘kimoyomoyo’ makosa yao yaliyotokana na ulevi wa mafanikio, wapinzani wao nao, Yanga inaonekana kama wanataka kuiga.
  Yanga wamemuacha kiungo hodari anayeweza kucheza kama beki pia, Salum Abdul Telela ‘Master’.
  Telela hajaongezewa Mkataba baada ya wa awali kumalizika mwishoni mwa msimu, licha ya umuhimu wake wa wazi unaoonekana katika timu kwa sababu ni kiraka anayeweza kucheza kama beki wa kulia, kati na nafasi zote za kiungo.
  Na kuhusu suala la nidhamu, Telela anaonekana ni mchezaji mwenye nidhamu, bidii ya mazoezi na kujituma, ambaye wakati wote anapoingizwa uwanjani licha ya muda mwingi kuwa mchezaji wa akiba hucheza vizuri. 
  Wachezaji wa Yanga wamesikitishwa na uamuzi wa kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm kumtema Telela, kwani licha ya ufundi wake kisoka, pia alikuwa rafiki wa kila mtu katika timu.
  Na hata baadhi ya viongozi wa Yanga bado wanapingana na uamuzi wa Pluijm kumtema Telela ambaye amedumu Yanga tangu mwaka 2011 aliposajiliwa mara ya kwanza kutoka Moro United.
  Swali, Telela anaachwa kwa sababu gani. Nidhamu, au Kiwango? Ametaka fedha nyingi katika Mkataba mpya? Hatujui.
  Yanga wasilichukulie kwa urahisi hili, kumuacha mchezaji aina ya Telela, mwenye uwezo, nidhamu na kujituma ni hatari, kwani itaanza kuwatia woga na wachezaji wengine, kwamba na wao iko siku wataachwa kama Salum ‘Abo Master’ bila kujali uwezo wao, juhudi na hata nidhamu.
  Bado najiuliza, Telela yule ninayemfahamu mimi ana matatizo gani? Mchezaji mkimya, mwenye bidii, nidhamu na utii na uwezo mkubwa pia kisoka, anaachwaje Yanga?
  Telela hana kinyongo, mpange, muweke benchi, ni yule yule tu. 
  Nakumbuka bao lake zuri katika mchezo wa Ngao ya Jamii Februari 23, mwaka 2013 likiipa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC na kuibua sherehe kubwa kwa mashabiki wa timu ya Jangwani. Nakumbuka ufundi wake uwanjani, nidhamu na upole wake. Lakini eti kaachwa Yanga. 
  Sababu? Hakuna, basi tu utashi sijui wa kocha au viongozi, lakini Yanga wajue Simba nao walianza kujibomoa taratibu kwa kufukuza wachezaji bila sababu za msingi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: UGONJWA WA SIMBA UNAPOANZA KUIINGIA YANGA TARATIBU! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top