• HABARI MPYA

    Saturday, June 11, 2016

    KAPUYA AWAPA SIMBA MBINU ZA USAJILI

    Na Somoe Ng’itu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa zamani wa Michezo Tanzania, Profesa Juma Athumani Kapuya amewashauri Simba waache kushindana na Azam na Yanga katika usajili.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo mjini Dar es Salaam, Kapuya amesema kwamba ni kweli kwa sasa Simba inazidiwa uwezo kiuchumi na Azam na Yanga, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kutopata wachezaji wazuri wa kusajili.
    “Kwanza nataka niwashauri jambo moja Simba, waache kushindana na Azam na Yanga. Wakati huu ambao Azam na Yanga wanasajili, wao watulie tu. Wawaache Azam na Yanga wasajili, naamini Azam na Yanga hawawezi kuwafikia wachezaji wote wazuri. Sasa wale watakaobaki ndiyo watakuja Simba kiulaini,”alishauri Kapuya ambaye ni mpenzi wa Simba.
    Waziri wa zamani wa Michezo, Juma Kapuya amewashauri Simba namna ya kusajili
    Pamoja na hayo, Kapuya alisema hafurahishwi na tabia ya sasa ya Simba kusajili  wachezaji chipukizi na kuwauza wanapokomaa, kipindi ambacho ndiyo wanatakiwa waanze kuisaidia timu.
    Ametoa mfano wachezaji waliosajiliwa wakiwa chipukizi kama beki Shomary Kapombe na kiungo Ramadhani Singano ‘Messi’ wote waliuzwa katika kipindi ambacho michango yao ilitakiwa kuanza kuonekana Simba.
    “Namna hiyo kila siku utakuwa unaanza upya. Lazima uongozi wa Simba uwe na uchungu na timu, uhakikishe wachezaji hawaondoki kwa urahisi. Lakini pia kuna suala la kuishi nao vijana ili wakati wote wafurahie kuwapo Simba, nalo viongozi wa Simba walitazame, wasijiruhusu kugombana gombana na wachezaji, na wahakikishe wanawatimizia ahadi, hapo wataishi nao vizuri,”alisema Kapuya.
    Waziri huyo amesikitishwa pia na desturi ya viongozi wa Simba kufukuza wachezaji wazuri kama ilivyowahi kutokea kwa viungo Amri Kiemba, Haroun Chanongo na washambulaji Elias Maguri na Amissi Tambwe na akawataka pia kuwa makini kutosajili wachezaji wenye mapenzi na mahasimu wao, kama Hassan Kessy.
    “Pia wawachunguze wachezaji kabla ya kuwasajili, ili wasije kurudia kusajili akina Kessy wengine hapa, lazima mchezaji ujue huko alipotokea alikuwa ana desturi zipi, ukitaka kujua utajua. Lakini ukikurupuka kumsajili bila kujua, ndiyo hivyo,”amesema Kapuya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAPUYA AWAPA SIMBA MBINU ZA USAJILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top