• HABARI MPYA

    Wednesday, October 14, 2015

    SOKA YA ZANZIBAR KIZANI, MAHAKAMA YAWAENGUA MADARAKANI VIONGOZI ZFA, KAMATI YA MUDA YAUNDWA

    Na Ameir Khalid, ZANZIBAR
    SIKU moja baada ya Mahakama Kuu ya Zanzibar kuwaamuru viongozi wa juu wa Chama cha Soka (ZFA) kuondoka madarakani, kamati ya muda kwa ajili ya kusimamia shughuli za chama hicho imeundwa.
    Juzi, Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mkusa Isaac Sepetu, wakati akisikiliza kesi inayowakabili viongozi hao, Rais wa ZFA Ravia Idarous, Makamu wake ofisi ya Pemba Ali Mohammed pamoja na Katibu Mkuu Kassim Haji Salum, alisema kwa mujibu wa katiba ya ZFA muda wao wa kukaa madarakani umemalizika hivyo wakae pembeni.

    Rais wa aliyeondolewa madarakani ZFA na Mahakama, Ravia Idarous kulia akiwa na rais wa zamani wa ZFA, Ali Ferej Tamim na Kocha Shaaban Ramadhani kushoto 

    Jaji Sepetu pia alitoa agizo la kuundwa kamati ya muda ya uongozi wa chama hicho ambacho mbali na kesi ya ubadhirifu wa fedha, inakabiliwa na kesi mbili za kukiuka katiba na kanuni za mashindano, zilizofunguliwa dhidi yake na klabu za Chuoni SC na Aluta.
    Kufuatia amri hiyo ya mahakama, Umoja wa Klabu za Soka Zanzibar umetaja kamati ya watu saba ambayo itakuwa na jukumu la kuweka mambo sawa ili shughuli za mpira wa miguu ziendelee, pamoja na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa chama hicho kupata viongozi wapya.
    Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa uwanja wa Amaan, Katibu wa umoja huo Ali Ussi Jongo, aliwataja walioteuliwa kuunda kamati hiyo kuwa ni Hussein Ali Ahmada anayekuwa Mwenyekiti ambapo Makamu wake atakuwa Omar Ahmed Awadh.
    Aidha, Hashim Salum Hashim anakuwa Katibu Mkuu akisaidiwa na Khamis Hamad, wakati Masoud Attai Masoud, Salum Hamdun na Ali Ussi Jongo wanakuwa wajumbe wa kamati hiyo.
    Jongo alisema miongoni mwa majukumu makubwa ya kamati hiyo ni kuzungumza na uongozi wa klabu za Chuoni SC na Aluta, kuziomba ziondoshe kesi walizoifungulia ZFA ili mpira uchezwe na ligi zianze.
    Aidha, alisema kazi nyengine ni kuandaa utaratibu wa kufanya uchaguzi mkuu wa chama hicho ambacho kwa muda sasa shughuli zake zimekwama kutokana na kuelemewa na mzigo wa kesi mahakamani.  
    Akizungumza na gazeti hili baada ya kuteuliwa kwake, Mwenyekiti wa kamati hiyo Hussein Ali Ahmada (pichani) ambaye pia ni Katibu wa kituo cha kukuza vipaji cha Oranje (OFA), alisema kazi waliyopewa ni ngumu lakini anaamini wakipata ushirikiano wataifanya kwa ufanisi mkubwa. 
    "Kwa kuwa nia yetu sote ni kuona soka linachezwa na kuendelea, na pia mimi nilikuwemo kwenye kamati ya usuluhishi kumaliza mzozo ndani ya ZFA, bila shaka kwa pamoja tutaweza kurejesha hali kuwa ya kawaida," alifafanua.
    Taarifa zaidi zilizopatikana na gazeti hili, zimefahamisha kuwa, ifikapo Jumamosi, mambo yote yanayokwamisha shughuli za ZFA yatakuwa yamemalizwa na kubaki kuwa historia.        
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SOKA YA ZANZIBAR KIZANI, MAHAKAMA YAWAENGUA MADARAKANI VIONGOZI ZFA, KAMATI YA MUDA YAUNDWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top