• HABARI MPYA

    Friday, February 24, 2012

    YANGA WAKATAFUTE BAO LA MAPEMA CAIRO

    JUMAMOSI Yanga ya Dar es Salaam ilijiweka katika mazingira magumu kuweza kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Zamalek ya Misri. Kwa matokeo hayo, Yanga sasa inatakiwa kushinda ugenini au itokee bahati kwao watoe sare ya zaidi ya 1-1, ili wasonge mbele kwa faida ya bao la ugenini kuhesabika mawili.
    Kwa sasa, hata sare ya 0-0, Zamalek inasonga mbele. Lakini ukweli ni kwamba kwa wenye kutambua rekodi ya Yanga dhidi ya timu za Misri, hawatarajii sare zaidi ya klabu hiyo kuendeleza rekodi yake ya kubebeshwa kapu la mabao inapocheza huko.
    Matokeo haya yenye kusononesha kwa wana Yanga, yanamaanisha kocha Mserbia wa klabu hiyo, Kostadin Bozidar Papic ameendeleza rekodi yake ya kushindwa kuing’arisha timu hiyo kwenye michuano ya Afrika.
    Hiyo ilikuwa mechi ya tatu Papic anaiongoza Yanga kwenye michuano ya Afrika bila kuondoka na ushindi, baada ya mwaka 2010 kufungwa mechi zote mbili za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Saint Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Ilifungwa 3-2 Dar es Salaam, kabla ya kwenda kumalizwa kwa kupigwa 1-0 Lubumbashi.
    Kwa ujumla, Yanga mara ya mwisho kushinda mechi ya Afrika ilikuwa Februari 14, mwaka 2009, ‘ilipoionea’ Etoile d Mironsty ya Comoro.
    Ikiwa chini ya Mserbia mwingine, Dusan Savo Kondic, Yanga ilifungwa mechi zote mbili na Al Ahly ya Misri mwaka 2009, ikipigwa 3–0 Cairo na 1-0 Dar es Salaam, katika Ligi ya Mabingwa.
    Kihistoria hiyo ilikuwa ni mechi ya tatu kuzikutanisha Yanga na Zamalek, awali mwaka 2000 zilimenyana mara mbili katika iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi Afrika.
    Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 5-1, ikilazimishwa sare ya 1-1 nyumbani, bao la wenyeji likitiwa kimiani na Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, kabla ya wageni kuchomoa kipindi cha pili.
    Wakati huo, Yanga ikifundishwa na Raoul Jean Pierre Shungu kutoka DRC, kikosini ikiwa na wakali kama Manyika Peter, Ally Mayay, Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu), Sekilojo Chambua na Edibily Lunyamila, ilifungwa 4-0 katika marudiano.
    Hata hivyo, siku hiyo kipa wa Yanga, Ismail Suma, alitolewa nje kwa kadi nyekundu, timu hiyo ikiwa nyuma kwa bao 1-0 na mshambuliaji Said Mhando (marehemu) akaenda kusimama langoni, ndipo mvua ya mabao ikawamiminikia.
    Lakini kwa ujumla Yanga haijawahi kuifunga timu yoyote ya Misri tangu ianze kukutana nazo mwaka 1982 kwenye michuano ya Afrika.
    Mwaka 1982 katika Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa, Yanga ilifungwa 5-0 na Al- Ahly mjini Cairo, kabla ya kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
    Mwaka 1988 Yanga ilifungwa 4-0 na Al Ahly katika Ligi ya Mabingwa, baada ya awali kulazimishwa sare ya bila kufungana Dar es Salaam.
    Mwaka 1992 Yanga ilitoa sare ya 1-1 na Ismailia mjini Cairo, bao lake likifungwa na Kenneth Pius Mkapa baada ya awali kufungwa 2-0 Dar es Salaam katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa.
    Mwaka 2009 Yanga ilifungwa na Al Ahly 1-0 Dar es Salaam ikitoka kufungwa 3-0 mjini Cairo katika Ligi ya Mabingwa na mwaka 2000 ilifungwa jumla ya mabao 5-1 na Zamalek katika Kombe la Washindi.
    Mwaka jana Yanga, ilicheza Kombe la Shirikisho na kutolewa Raundi ya Kwanza tu na Dedebit ya Ethiopia kwa kufungwa jumla ya mabao 6-4, ikitoa sare ya 4-4 Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 2-0 Addis Ababa.
    Mafanikio makubwa kwa Yanga katika michuano ya Afrika ni kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa 1998, na wakati michuano hiyo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika, walicheza Robo Fainali mara mbili 1969 na 1970 na walifika pia Robo Fainali ya Kombe la Washindi mwaka 1996.
    Baada ya matokeo ya Jumamosi, wengi wameelezea mitazamo yao kuhusu mchezo huo wa kwanza na zaidi lawama zinaelekezwa kwa kocha Kostadin Bozidar Papic na washambuliaji Kenneth Asamoah na Davies Mwape.
    Papic analaumiwa kwa nini aliendelea kuwaacha uwanjani Asamoah na Mwape hata baada ya kugundua wameshindwa kuisaidia timu na washambuliaji hao nao wanalaumiwa kwa kukosa mabao ya wazi, ambayo mwisho wa siku yaliigharimu timu.
    Kwa sasa tunaweza kuendelea na mjadala huu wa nani anastahili lawama kwa matokeo ya Jumamosi, kwa sababu hiyo ni desturi yetu Watanzania kuangalia tunapoangukia na si tulipojikwaa.
    Ndiyo, Papic alifanya uzembe kwa kutowatoa wachezaji ambao walishindwa kuisaidia timu. Hakuna ubishi na hilo linadhihirishwa na kile alichokifanya mwenzake, Hassan Shehata wa Zamalek, alifanya mabadiliko mapema sana baada ya kuona mambo hayaendi vizuri.
    Mwape na Asamoah walikosa mabao, ndiyo wanastahili lawama, si walikosa kweli.
    Lakini pamoja na mtazamo huo, umefika wakati sasa tujiulize tutaendelea na desturi ya kutafuta wachawi na kulaumiana baada ya matokeo mabaya hadi lini?
    Matatizo ya Papic yalikuwa yanajulikana Yanga hata kabla hajarejeshwa kwamba ni kocha asiyeshaurika na anayejiamini kupita kiasi na pia ni mtu asiyejali.
    Inastaajabisha leo viongozi wa Yanga kusema wanataka kususa iwapo hatafukuzwa kwa sababu hashauriki na ni mbabe. Inawezekana Yanga kukosa ushindi Jumamosi, Papic ni sehemu ya sababu, tena ndogo tu, lakini kuna sababu za msingi ambazo zinabeba mustakabali wa Yanga kwenye soka yake.
    Papic si kocha wa kwanza anashindwa kuifunga timu ya Misri - na hakuna kocha aliyewahi kuiongoza Yanga kuifunga timu ya nchini humo. Hajawahi kutokea.
    Mimi naamini, Boniphace Ngairah Ambani alikuwa bora kuliko mshambuliaji yeyote wa Yanga hivi sasa - lakini alishindwa kufunga hata bao moja timu hiyo ikicheza na Al Ahly katika mechi zote mbili.
    Naamini pia, Yanga ya 2009/2010 ilikuwa nzuri zaidi ya hii sasa kwa maana ya timu, lakini ilishindwa kuifunga Ahly.
    Leo kinachoendelea Yanga kinaweza kuathiri hata maandalizi ya mechi ya marudiano dhidi ya Zamalek. Huu si wakati wa kutupiana lawama, badala yake kila mtu abebe jukumu lake na timu iingie kwenye maandalizi ya msingi ya mchezo wa marudiano.
    Hakuna ambacho Zamalek waliacha katika mchezo wa Jumamosi, walicheza kwa uwezo wao wote kutafuta matokeo mazuri, ingawa kidogo refa alikuwa upande wa wenyeji.
    Yanga wamebahatika kuijua Zamalek ya sasa na katika mchezo wa marudiano watakwenda kucheza na timu wanayoijua tofauti na huu wa kwanza, walikutana na timu wanayoisikia tu. Kadhalika Zamalek nao sasa wanaijua Yanga.
    Kama alivyosema Shehata, mchezo wa marudiano utakuwa mgumu, kweli utakuwa mgumu.
    Jambo moja tu kama silaha yao Yanga, wanatakiwa kwenda kutafuta bao la mapema ugenini ili kuwachanganya wageni.
    Wakijipanga inawezekana. Lakini kama wataishia kulumbana na kunyoosheana vidole, siku zitakatika na wataingia kwenye mchezo wa marudiano kwa ajili ya kukamilisha ratiba tu. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAKATAFUTE BAO LA MAPEMA CAIRO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top