• HABARI MPYA

    Tuesday, February 28, 2012

    STARS NA MAMBAZ NI PATASHIKA KESHO


    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kesho inatarajiwa kuvaana na Msumbiji, Mambas katika mchezo wa kwanza wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini.
    Timu hizo zitarudiana mjini Maputo na mshindi wa jumla ataingia raundi ya mwisho ya kufuzu, akimenyana na moja ya timu zilizoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 2012.
    Raundi ya mwisho ya kufuzu itafanyika kati ya Septemba na Oktoba kuamua timu zitakazocheza fainali za mwakani za Afrika Kusini.
    Kocha wa Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Jan Borge Poulsen atashusha kikosi chake leo, akitoka kutoa sare nyumbani katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Jumatano iliyopita.
    Baada ya sare hiyo, Poulsen alilaumiwa kwa kutomuita chipukizi anayeinukia vizuri, Mbwana Ally Samatta kwenye kikosi chake, ingawa ameendelea kutetea uamuzi wake kwa kusema mchezaji huyo hajitumi akiwa na jezi ya timu ya taifa.
    Pamoja na utetezi huo, Poulsen alikiri ana tatizo katika safu ya ushambuliaji, ambayo inaundwa na wachezaji chipukizi pia, John Bocco wa Azam FC na Hussein Javu wa Mtibwa Sugar.
    Lakini Poulsen alisema amefurahishwa na safu ya ulinzi ilivyocheza dhidi ya DRC na ana matumaini nayo kuelekea mchezo wa leo.
    Msumbiji wanashuka kwenye Uwanja wa Taifa, wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuwafunga wenyeji mechi mbili mfululizo kwenye Uwanja huo.
    Novemba 19, mwaka 2008  katika mchezo wa kirafiki Mambas waliipa Tanzania bao 1-0, enzi hizo ikinolewa bado na Mbrazil Marcio Maximo na Septemba 8, mwaka 2007 walishinda 1-0 katika mchezo wa tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Matafia yua Afrika.
    Katika mechi mbili zilizochezwa Maputo pia, moja timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana Oktoba 7, mwaka 2006 katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na mwingine Aprili 23, mwaka jana Msumbiji walishinda 2–0, tayari Poulsen kocha wa Stars.
    Poulsen aliyeanza kazi vizuri Tanzania kwa kuipa Bara, Kombe la Challenge mwaka juzi, anakabiliwa na shinikizo la kushinda mechi ya leo, haswa baada ya timu hiyo kufungwa 1-0 nyumbani mara ya mwisho na Chad katika mchezo wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia Novemba 15, mwaka jana.
    Mdenmark huyo, aliyekuwapo kwenye benchi la ufundi wakati Denmark inatwaa Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 1992 wengi wanatakia aachie ngazi iwapo matokeo yatakjuwa mabaya leo, hali ambayo itamfanya atumie ‘uchawi’ wote kunusuru kibarua chake leo.
    Katika mchezo wa leo, Poulsen anatarajiwa kutumia idadi kubwa ya wachezaji aliowatumia kwenye mechi na DRC wiki iliyopita.
    Stars: Juma Kaseja, kulia Nahodha Nsajigwa Shadrack, Stefano Mwasyika, Kelvin Yondan, Aggrey Moriss, Shaaban Nditi, Uhuru Suleiman, Abdi Kassim, John Bocco, Mrisho Ngassa na Vincent Barnabas.

    REKODI YA TANZANIA NA MSUMBIJI:
    Aprili 23, 2011
    Msumbiji 2 – 0 Tanzania
    Novemba 9, 2008
    Tanzania 1 – 0 Msumbiji
    Septemba 8, 2007
    Tanzania 0 – 1 Msumbiji
    Oktoba 7, 2006
    Msumbiji 0 – 0 Tanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS NA MAMBAZ NI PATASHIKA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top