• HABARI MPYA

    Sunday, February 19, 2012

    TUENDELEE NA FOOTBALL FITINA, AU?

    MWAKA 2005 Tanzania ilifuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, baada ya kuzitoa Rwanda katika Raundi ya Kwanza, Zambia katika raundi ya Pili na Zimbabwe katika Raundi ya Tatu.
    Hata hivyo, likatokea tatizo; utata kuhusu umri halisi wa kiungo anayeweza kucheza nafasi za ulinzi pia, Nurdin Hamadi Bakari ambaye wakati huo alikuwa mchezaji wa Simba SC. Simba iliwasilisha usajili wake kwa ajili ya michuano ya Afrika, ikionyesha Nurdin anazidi miaka 17 na kwa maana hiyo hastahili kuchezea timu ya vijana wa umri huo.  Kwa sababu aliichezea Tanzania katika michuano hiyo ya vijana na Zambia na Zimbabwe zilikata rufaa, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likaiondoa nchi yetu kwenye michuano hiyo na Zimbabwe wakapewa nafasi yetu. Pamoja na Nurdin, wachezaji wengine waliokuwa wanaunda timu hiyo ni kama Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan, Juma Jabu, Amir Maftah, Omar Matuta ‘Wanchope’ na wengineo. Kijana aliyekuwa ana umri wa miaka 17 mwaka 2005, maana yake leo atakuwa ana umri wa miaka 23- je, tukiwatazama akina Nizar, Matuta, Jabu, Maftah na Nurdin walivyo sasa, ni kweli wana miaka 23? Tukubali tulidanganya. Tulidanganya ili tuwe na timu ya ushindani ituletee matokeo mazuri wakati huo. Tuliyapata, bahati mbaya tu mkanganyiko wa Nurdin ulituharibia mambo, vinginevyo timu ingeshiriki fainali za Gambia. Miaka saba baadaye, wachezaji wa U17 ya Zambia, Rwanda na Zimbabwe waliotolewa na U 17 yetu ndio leo wanaibeba soka ya nchi yao. Kwa sasa ukipigisha kura za kuchagua wachezaji vijana Tanzania, kwa wapenzi wengi wa soka nchini hawatawapigia akina Chuji, Nurdinm, Matutam, Jabu wala Nurdin- lakini kwa nini na hawa hawazidi miaka 23? Wakubwa wana jibu. Nina uhakika wana jibu, kwa sababu wao ndio wana ukweli juu ya timu zao za vijana wanazounda. Tulidanganya. Na tuliona wajanja kweli wakati huo, tukizifunga kwa kuzizidi uwezo Rwanda, Zambia na Zimbabwe. Lakini leo ikiwa miaka saba baadaye tangu tujione wajanja kwa kudanganya, hapana shaka tumekwishaanza kugundua kwamba, tulijidanganya.  Kama tulichekelea wakati tunazitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe kwa ujanja wetu, huu sasa ni wakati wa kujicheka kwa ujinga wetu. Wenzetu walifuata dhana halisi ya mashindano ya vijana, ambayo ni kumuandaa mchezaji hodari wa kesho na hatimaye leo wamefanikiwa vijana wao wamewabeba na wamewapa ubingwa wa Afrika. Sisi vipi? Tuna nini? Iko wapi faida ya ujanja wetu leo?  Kwa kuwa desturi ya kujidanganya imeendelea hata baada ya timu ile iliyoenguliwa na CAF, nataka niwaambie wakubwa- hatutafanikiwa daima kwa mtindo huo. Katika kumuandaa mchezaji bora wa baadaye, lazima apitie katika hatua mbili muhimu; kwanza kumuibua, pili kumuendeleza. Kuibua wachezaji, tunafanikiwa sana kwa sababu tuna vyanzo vya kutosha hivi sasa. Mashindano ya vijana ni mengi nchini, kuanzia ya shule, Copa Coca Cola na hata ya mitaani, tatizo moja tu desturi ya kudanganya umri inatia doa mashindano kwa timu nyingi kupeleka wachezaji waliozidi umri. Mashindano mengi ya U17 yanashirikisha vijana wenye umri wa miaka 20 au zaidi, matokeo yake hadi mchezaji kufikia kwenye kiwango cha kucheza timu ya taifa ya wakubwa, baada ya miaka miwili au mitatu tu anakuwa amekwishachoka. Lakini kama tutafanikiwa kupambana na mtihani wa kudanganya umri, kwa kuyapa fursa mashindano yetu ya vijana kushirikisha wachezaji wenye umri halisi uliotajwa kwenye kanuni, tutakuwa tumevuka kikwazo cha kwanza katika kumtayarisha mchezaji bora wa baadaye.    Jambo la pili, ambalo ni muhimu zaidi na kwa kiasi kikubwa hapa ndipo tumekuwa tukipotezea wachezaji wengi, ni jinsi ya kumuendeleza mchezaji baada ya kumuibua. Ilipokuwa TSA (Tanzania Soccer Academy) wengi tuliamini hii itasaidia, lakini ajabu wakubwa wakaiua. Tena bila sababu ya msingi. Baada ya kumuibua mchezaji, lazima annadaliwe, aendelezwe, alelewe katika misingi ya maadili ya soka, apewe elimu ya kujitambua, ili ajenge ndoto.  Lazima mtoto ajitambue na ajiwekee malengo, hivi ni vitu ambavyo akina Yaya Toure walipitia wakiwa akademi ya ASEC Mimosas. Hivi ni vitu ambavyo akina Robin Van Persie walipitia wakiwa akademi ya Fayernood. Ernest Mokake (sasa marehemu) alifanya kazi kubwa ya kuibua vipaji vya vijana miaka ya 1990 mwishoni hadi 2000 mwanzoni. Miongoni mwao ni Haruna Moshi. Kama miujiza ya Mungu itatokea, Mokake akarejea duniani leo na kukutanishwa na Haruna Moshi, hapana shaka atamkana. Atasema huyu si Haruna yule niliyekuwa naye U17. Haruna aliibuliwa, lakini akakosa mwendelezo mzuri wa kimaadili na matokeo yake, amekuwa Haruna huyu ambaye tunaye leo. Alaumiwe nani? Hata Yaya, kama baada ya kuibuliwa angeachwa tu akue ovyo, sijui kama angekuwa Yaya huyu ambaye tunamshuhudia leo, mwanasoka bora mwenye nidhamu na mafanikio makubwa. Hakuna hakika. Tayari wale vijana wa Copa Coca Cola waliokwenda Brazil na Afrika Kusini na kufanya vizuri, hatujui wanaendelezwaje- kwani hawakuwekewa misingi ya kuendelezwa. TSA imekufa na tumepoteza mno. Kipi kinabeba matumaini yetu kwa sasa? Leo Watanzania wanalia na kusikitika Zambia imekuwa bingwa wa Afrika, wakati wao hata kufuzu ni ‘ishu’. Mbali mno kuifikiria Zambia, kwa sababu wao wana mipango endelevu na thabiti, tena ya tangu enzi. Ndiyo maana mwaka 1993 baada ya wachezaji wake wote wa kikosi cha kwanza kufariki ajalini pwani ya Gabon, waliunda timu nyingine ambayo ilifika Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika na kufungwa kwa tabu na Nigeria 2-1. Sisi labda tuumizwe na Sudan, ambayo kila siku tunagalagala nayo kwenye mashindano ya CECAFA, lakini si Zambia wenye mipango yao na wanaojua nini wanakifanya katika soka. Wakubwa wanaamini football fitina. Acha waendelee kuamini kwa kuwa hiyo ndiyo dira yao, lakini watambue ni potofu. Kwa sasa mchakato wa mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Copa Coca Cola ndio umeanza. Unapozifikiria fainali za Kombe la Dunia 2018 Urusi, lazima kwanza ufikirie Copa Coca Cola ya mwaka huu. Jinsi gani utaibua vipaji, jinsi gani utaviendeleza ili mwaka 2018 upate timu ya kukupa tiketi ya Kombe la Dunia.  Kwa wataalamu wa michakato ya football fitina, hapa ni kiza tu na 2018 itafika na hadithi itabaki kuwa ile ile. Ila kwa wataalamu, wenye kuendesha mambo kitaalamu kwa kufuata misingi ya kitaaluma, mambo yatakuwa mazuri. Sasa tuamue, tuendelee na football fitina, au? Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUENDELEE NA FOOTBALL FITINA, AU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top