• HABARI MPYA

    Saturday, February 25, 2012

    NGASSA WA HAPA HAPA TU

    KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa, sasa hatajiunga tena na Seattle Sounders ya Ligi Kuu ya Marekani, baada ya kile kilichoelezwa nafasi yake imechukuliwa na mchezaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo (DRC.)   Rahim Kangezi ‘Zamunda’, aliyemtafutia Ngassa nafasi ya kujaribiwa Seattle mwaka jana, alisema jana mjini Dar es Salaam kwamba Mkongo huyo ambaye naye alifanya majaribio Seattle, alimvutia zaidi kocha wa timu hiyo, Sigi Schmid, ambaye akapendekeza achukuliwe kwanza kabla ya Ngassa.
    Hata hivyo, Zamunda alisema Ngassa bado anafikiriwa na Seattle na ikitokea nafasi nyingine ataitwa kwenda kutimiza ndoto zake za kucheza ‘majuu’.
    Hii ni mara ya pili, Ngassa anafanya majaribio ‘majuu’ na kuambiwa amefuzu, lakini hachukuliwi.
    Awali, Aprili mwaka 2009, Ngassa alifanya majaribio katika klabu ya West Ham United ya England na ikaelezwa amemvutia aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, wakati huo klabu hiyo ikiwa Ligi Kuu, Gianfranco Zola.
    Lakini ilielezwa Ngassa ambaye wakati huo alipelekwa na Yussuf Bakhresa England, alitakiwa kureja Afrika kujenga mwili, ingawa ‘ndio imetoka hadi kesho’.
    Julai mwaka jana, iliripotiwa kwamba Ngassa alifuzu majaribio alipokuwa Marekani na soka yake ilimkosha mno Kocha Mkuu wa Sounders, Sigi Schmid. 
    Mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, katika majaribio yake Seattle, alipewa nafasi ya kucheza katika mechi ya kirafiki dhidi ya Manchester United ya England kwa dakika 14, siku hiyo Sounders ikifungwa mabao 7-0.
    Katika mechi hiyo, Ngassa alikaribia kufunga bao baada ya kumzidi ujanja Rio Ferdinand, lakini kwa bahati mbaya shuti lake ‘lilipotea njia’.
    Ngassa aliyezaliwa Mei 5, mwaka 1989 mjini Mwanza, alijiunga na Azam FC Mei 21, mwaka jana akitokea Yanga kwa dau la jumla ya Sh milioni 108.
    Kwa sasa Ngassa cheche zake zimepungua katika soka ya Tanzania kiasi kwamba hata kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen amesema anampa nafasi ya mwisho ya kuthibitisha uwezo wake katika kikosi kitakachoivaa Msumbiji Jumatano.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGASSA WA HAPA HAPA TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top