• HABARI MPYA

    Wednesday, February 29, 2012

    STARS SARE NA MSUMBIJI, YAJIWEKA PAGUMU AFCON 2013

    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo imeanza vibaya kampeni za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na msumbiji, Mambas kwenye Uwanja wa taifa, Dar es Salaam.
    Mambas ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza katika mechi hiyo katika dakika ya 22, lililofungwa na Clesio Bauque baada ya kutumia vizuri uzembe uliofanywa na mabeki wa Stars.
    Stars walisawazisha bao hilo kupitia kwa Mwinyi Kazimoto katika dakika ya 41 baada ya kupokea pasi ya Vicent Barnabas kabla ya kuachia shuti kali nje ya 18 lililokwenda moja kwa moja wavuni.
    Kwa matokeo hayo, Stars inatakiwa lazima kushinda ugenini au kutoa sare ya zaidi ya bap 1-1 ili kusonga mbele katika kuwania tiketi ya kucheza fainali za AFCON mwakani.
    Timu hizo zitarudiana mjini Maputo na mshindi wa jumla ataingia raundi ya mwisho ya kufuzu, akimenyana na moja ya timu zilizoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 2012.
    Raundi ya mwisho ya kufuzu itafanyika kati ya Septemba na Oktoba kuamua timu zitakazocheza fainali za mwakani za Afrika Kusini.
    Kikosi hicho cha Kocha wa  Mdenmark Jan Borge Poulsen leo kinatoa sare ya pili mfululizo kwenye Uwanja wa nyumbani, baada ya wiki iliyopita kutoka 0-0 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kirafiki.
    Mashabiki walimlaumu kwa mara nyingine Poulsen kwa kutomuita chipukizi anayeinukia vizuri, Mbwana Ally Samatta wa Tout Puissant Mazembe ya DRD.
    Sare hiyo inaifanya Msumbiji ilinde rekodi yake ya kutofungwa kwenye Uwanja wa Taifa. Novemba 19, mwaka 2008  katika mchezo wa kirafiki Mambas waliipa Tanzania bao 1-0, enzi hizo ikinolewa bado na Mbrazil Marcio Maximo na Septemba 8, mwaka 2007 walishinda 1-0 katika mchezo wa tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Matafia yua Afrika.
    Katika mechi mbili zilizochezwa Maputo pia, moja timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana Oktoba 7, mwaka 2006 katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na mwingine Aprili 23, mwaka jana Msumbiji walishinda 2–0, tayari Poulsen kocha wa Stars.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS SARE NA MSUMBIJI, YAJIWEKA PAGUMU AFCON 2013 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top