• HABARI MPYA

    Friday, February 24, 2012

    YANGA NA ZAMALEK BILA MASHABIKI UWANJA WA JESHI

    UWANJA wa Jeshi wa Arab Contractors jijini Cairo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 22,000, ndio utakaokuwa mwenyeji wa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Zamalek dhidi ya Yanga hapo Machi tatu.
    Utata kuhusu wapi itakapochezwa mechi hiyo ya marudiano ilitokana na vurugu zilizotokea Misri kwenye uwanja wa Port Said na kusababisha watu 74 kupoteza maisha wakati wa mechi ya Ligi Kuu nchini humo kati ya Ahly dhidi ya Al Masry.
    Kutokana na hali hiyo Zamalek walisema kama serikali itashikiria uamuzi wa kuzuia mechi za soka kuchezwa nchini Misri watalazimika kucheza mechi yao ya marudiano na Yanga nje katika nchi ya Algeria au Sudan.
    “Tunatumaini tutafahamu vizuri kuhusu hali ya usalama hapa na kama serikali itatupa ruhusu ya kucheza mchezo wetu hapa au laa,” alisema msemaji wa Zamalek, Ali Aboul-Naga Said.
    Zamalek imepokea maombi kutoka klabu ya Algeria, ES Setif na Hilal ya Sudan kuwa wenyeji wa miamba hiyo ya Cairo inayopewa nafasi ya kusonga mbele baada ya kupata sare ya 1-1 ugenini Jumamosi iliyopita.
    Lakini, jana serikali ya kijeshi ya Misri ilitoa ruksa kwa Zamalek kucheza mechi hiyo nyumbani kwenye uwanja wa chuo cha jeshi uliojengwa mwaka 1989 kwa lengo la kutumika kwa michezo ya majeshi pekee ukiwa kwenye Mtaa wa Onouba kaskazini mwa jiji la Cairo umbali wa maili 7 kutoka uwanja wa kimataifa wa Cairo.
    Baadhi ya wachezaji wa Yanga wamesema wapo tayari kukabiliana na Zamalek katika nchi yoyote kwenye mchezo wao wa marudio.
    Mechi hiyo itachezwa bila ya mashabiki kutokana na Shirikisho la Soka Afrika, CAF kuwafungia mashabiki wa Zamalek kutokana na vurugu walizofanya kwenye mchezo dhidi ya Club Africain ya Tunisia uliofanyika mwaka jana kwenye uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
     Zamalek ilitwaa ubingwa mara ya mwisho wa Afrika mwaka 2002, wiki iliyopita ili nusurika kipigo baada ya kupata sare ya 1-1 na Yanga kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam.
    Hata hivyo, Zamalek wanategemea kurejea kwa wachezaji wake majeruhi katika mchezo huo kutawafaidia watapocheza dhidi ya Yanga hapo Cairo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA NA ZAMALEK BILA MASHABIKI UWANJA WA JESHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top